Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti kuhusu hali ya mgongano kati
ya Kamati ya Utendaji ya TFF na Bodi ya ligi Tanzania (Tanzania Premier league
Board).
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania linapenda kutoa ufafanuzi
ufuatao:
1.Bodi ya ligi imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF kifungu
40(11).Hivyo Bodi ya ligi ni zao la Mkutano Mkuu wa TFF.
2.Katiba ya TFF imeipa mamlaka kamati ya utendaji ya
TFF kutunga kanuni za uendeshaji wa Bodi ya ligi,kanuni hizi ndiyo nguzo kuu ya
uendeshaji wa shughuli za Bodi ya ligi na ndizo zinaipa Bodi uhalali wake wa
kuendesha shughuli zake za kila siku.
3.Bodi ya ligi ni chombo cha TFF kama vilivyo vyombo vingine
vikiwemo kamati mbali mbali za TFF.Kisheria Bodi ya ligi sio chombo huru (its
not a legal entity) hivyo Bodi pamoja na mambo mengine haina mamlaka ya kuingia
mikataba ya aina yoyote ya kisheria .
4.Katiba ya TFF inatamka kuwa Bodi ya ligi itaheshimu na kufuata
maagizo ya TFF.Maagizo haya yanatolewa na Sekretarieti ya TFF kwa niaba ya kamati
ya utendaji ya TFF.
5.Mwenye mamlaka ya kutengua maamuzi ya kamati ya utendaji ya TFF
ni Mkutano Mkuu wa TFF peke yake,hakuna chombo kingine cha chini chenye mamlaka
hayo.
6.Kanuni za mashindano zinaandaliwa na kamati ya mashindano ya TFF
na kupitishwa na kamati ya utendaji ya TFF. Kikao cha kamati ya utendaji
kilichopitisha rasimu ya kanuni za ligi za mwaka 2014/15 kilihudhuriwa na
Mwenyekiti wa bodi ya ligi,Makamu mwenyekiti wa Bodi ya
ligi na pia Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya TFF,hawa wote ni wajumbe wa
Bodi ya ligi na walishiriki kikamilifu katika kikao cha kamati ya utendaji
kilichopitisha kanuni za ligi 2014/15 ukiwemo na utaratibu wa mgawanyo wa
mapato ya milangoni na ya udhamini.Katiba ya TFF inaagiza hivyo kuwa
Viongozi wakuu wa Bodi ya ligi watakuwa pia ni wajumbe wa kamati ya
utendaji ya TFF. Aidha mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi alikuwepo kwenye kikao
hiki cha kamati ya utendaji kama mwajiriwa.
7. Uamuzi wa kuunda mfuko maalum wa kuendeleza soka la vijana ni
uamuzi uliopitishwa na kamati ya utendaji.Lengo la kuanzishwa mfuko huu ni kuwa
na chombo maalum ambacho kitakuwa kinakusanya fedha toka vyanzo mbali mbali kwa
ajili ya kuendeleza miradi ya soka la vijana nchini.Kwa sasa miradi hii ni:
(a) Kuanzisha vituo vya kulea na kuendeleza vipaji vya watoto
kuanzia miaka 8-17 (sports centres) katika kila mkoa nchini
mwetu.Mradi huu ni mkubwa utahitaji nyenzo hasa walimu na vifaa.
(b) Kuandaa timu ya taifa umri chini ya miaka 12 kwa
ajili ya mashindano ya Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Timu hii
itaanza kuandaliwa mwaka huu Desemba baada ya mashindano ya kitaifa umri chini
ya miaka 12. Hii timu itakusanywa na kuwekwa katika shule moja ya bweni ambapo
watalelewa na kuendelezwa vipaji vyao wakiwa pamoja huku wanasoma.Tanzania
tumeomba kuwa wenyeji wa fainali hizi.
(c) Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 14 kwa ajili ya
michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini ya miaka 17
mwaka 2017.
(d) Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 17 kwa ajili ya
michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini ya miaka 20
mwaka 2017.
(e) Kuandaa mashindano ya Taifa ya mpira wa wanawake na ligi ya
taifa ya mpira wa wanawake.
Miradi yote hii muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania
haina udhamini lakini ni lazima ifanyike ili tujihakikishie tunainua mpira
nchini mwetu.Mafanikio ya miradi hii sio tu yatafaidisha na kuimarisha timu
zetu za Taifa lakini pia yatakuwa chimbuko madhubuti la wachezaji
mahiri wa vilabu vyetu vya mpira wa miguu.
Kimsingi tunatarajia kuwa vyanzo vikuu vya mapato ya kutunisha
mfuko wa maendeleo ya mpira Tanzania vitakuwa:
- Mapato yatokanayo na
mechi za ligi zetu madaraja yote
- Mapato yatokanayo na
mechi za kimataifa
- Wadhamini
- Serikali kuu kupitia
bajeti za Wizara zenye dhamana ya michezo,halmashauri na vyuo
- Wafadhili
- Shughuli mbali mbali
za kutunisha mfuko.
Kamati
ya utendaji ya TFF ilimteua Bwana Leodeger Tenga kuwa mwenyekiti wa kwanza wa
mfuko huu na wajumbe wake ni Bw Tarimba Abbas, Bw Ephraim Mafuru, Mzee Ayoub
Chamshama Bw Frederick Mwakalebela na Mh Zarina Madabida. Bw Henry
Tandau na Bw Boniface Wambura ni waratibu wa mfuko huu. Imani ya TFF ni kuwa
wajumbe hawa kwa kutumia uzoefu wao katika uongozi wa jamii watatusaidia
kuhakikisha mfuko huu unaanza vyema shughuli zake.
Upande
wa TFF tumefungua akaunti maalum benki kwa ajili ya kuingiza fedha zote zinazokusanywa
kama mchango wa TFF kwenye mfuko huu zikiwemo asilimia 5 za makato ya fedha za
udhamini na ZILE zitokanazo na mfuko wa jichangie,TFF inatoa wito kwa wadau
wote wa mpira wa miguu Tanzania kuchangia mfuko huu ili utumike kunusuru mpira
wetu. Fedha zitakazokusanywa matumizi yake yatasimamiwa na kanuni za
uendeshwaji wa mfuko huu.
Hitimisho:
Kila
mwanafamilia wa TFF anawajibika kuheshimu na kufuata maelekezo ya
Kanuni za mashindano ya ligi kuu kama zilivyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya
TFF .Hivyo utaratibu wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na fedha za
milangoni na za wadhamini kama ulivyoainishwa kwenye kanuni hizi uko pale pale.
Ninaiagiza Bodi ya ligi kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya utendaji
ya TFF mara moja. Mwenye malalamiko kuhusu kanuni hizi ayalete
kwenye vyombo husika vya TFF kwa kufuata Katiba,kanuni na taratibu
za Shirikisho.Sote tunajenga nyumba moja hakuna haja ya kugombea fito.
Jamal
Malinzi
0 COMMENTS:
Post a Comment