Na Saleh Ally
MWAKA 2009 nikiwa jijini
Abidjan, Ivory Coast, nilikutana na mshambuliaji niliyetambulishwa kwake kwa
jina la Wilfred Bony ambaye wakati huo alikuwa akikipiga katika timu ya Sparta
Prague ya nchini Czech.
Dereva teksi niliyekuwa
nikitembea naye, alinieleza hadithi yake nzuri kwamba alitokea katika klabu
ndogo ya Issia Wazi iliyosifika kwa kuibua vipaji lakini pia ilisifika sana kwa
ukabila.
Kilichonivutia ni kwamba
Bony aliwahi kufeli majaribio katika Klabu ya Liverpool ya England na wananchi
wengi wa Ivory Coast waliamini ndiye atakayekuja kuwa Drogba mpya kwa kuwa
alizitesa sana timu kongwe za Asec Mimosa na African Sports kwa muda mfupi
aliochezea Issia Wazi.
Nilimsogelea Bony, nikazungumza
naye ikiwa ni baada ya kujitambulisha. Yalikuwa mazungumzo ya kawaida tu si
mahojiano. Kabla ya kuachana niliomba kupiga naye picha, akanitolea nje.
Akaniambia: “Bado mimi si
nyota, hauhitaji kupiga picha nami.”
Awali nilidhani anatania,
lakini baadaye alishikilia msimamo wake hadi mechi kati ya DR Congo na Ghana
ilipoanza katika Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny kidogo sikufurahia, lakini
niliamua kuheshimu msimamo wa mshambuliaji huyo ambaye nilielezwa alirudi Ivory
Coast.
Miaka minne baadaye, nilikutana
na Bony jijini Dar es Salaam. Alikuwa amekuja na kikosi cha Ivory Coast kuivaa
Taifa Stars. Nilifika katika hoteli waliyofikia baada ya appointment yangu na kocha
Sabri Lamouch kuzaa matunda. Pia niliomba mahojiano na Yaya Toure, lakini siku
hiyo aligoma hata kutoka chumbani akisisitiza alikuwa ana ‘focus’ kuhusiana na
mechi dhidi ya Stars.
Baada ya mahojiano na
Lamouch, nilimuona Bony akipita, nilimsimamisha na kumkumbusha mazungumzo yetu
kule Abidjan. Kwa mara ya kwanza niligundua hakuwa akiringa kama nilivyofikiri.
Kwanza alicheka sana,
akasema amefurahishwa kukutana nami. Nikamuuliza vipi kuhusu picha, haraka
alikubali na tulipomaliza kupiga picha, akaniambia. “Bado sijawa staa, ndiyo
naanza mbio za kuwa staa.”
Baada ya hapo aliingia
kwenye basi la wachezaji ili kuanza safari ya kwenda Uwanja wa Taifa kuivaa
Taifa Stars katika mechi ambayo wageni hao walishinda kwa mabao 4-2, Bony
akifunga la nne dhidi ya kipa Juma Kaseja.
Leo Bony, 26, Swansea
wamekubali kumuuza kwenda Manchester City kwa kitita rundo cha pauni milioni 30
(Sh bilioni 81) na mshahara mnono wa pauni 100,000 (Sh milioni 270) kwa wiki.
Aisee, ninawaza mambo mengi sana, ninajifunza lakini nawatupia wote tutafakari.
Afrika Magharibi ina
wachezaji wengi waliofanikiwa kwa kuwa wana uwezo wa kujaribu, wanataka kufanya
vema na si waoga kujaribu. Jiulize wachezaji wa hapa nyumbani wanafanya hivyo?
Huenda ni tabia ya
Watanzania wengi, hawajiamini na si watu wanaopenda bugudha. Wanataka mambo
yaende kiulaini ndiyo maana wengi wanacheza hapa nyumbani tu!
Wakati Bony anakataa kupiga
picha nami kwa kigezo kuwa yeye si staa, alikuwa akimaanisha. Siku alipokubali
kupiga picha alisisitiza, bado hajawa staa. Lakini sasa hakuna ubishi kuwa ni
staa na kweli anastahili kuwa mrithi wa Drogba kama wapenda mpira wa Ivory
Coast walivyoamini miaka zaidi ya mitano iliyopita.
Kweli Jonas Mkude anataka
kujaribu hiyo, vipi kuhusu Frank Domayo na Simon Msuva? Wote wanasubiri jua la
jioni ndiyo waanze kufanya mipango ya kwenda Ulaya?
Wote wanasubiri hadi wapate
maudhi, wadharauliwe au kukasirishwa na viongozi wa Simba, Yanga au Azam FC
ndiyo wafikirie ni wakati mwafaka kutoka nje ya Tanzania?
Wapo wachezaji wengi wenye
uwezo wa kucheza angalau Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya Magharibi kama
ambavyo Bony alifeli England akaenda Jamhuri ya Czech, halafu akarudi na baada
ya kufanya vema Swansea, sasa anatua kwenye kikosi cha mabingwa wa England.
Tuache maneno mengi, jamani amkeni.
0 COMMENTS:
Post a Comment