HII haitakuwa ni mara ya
kwanza kuandika kuhusiana na namna Mtibwa Sugar wanavyofanya mambo yao kwa
mfumo wao wa kipekee, nikaeleza wazi kuwa unanivutia.
Nakumbuka mara ya mwisho
nilizungumzia namna ambavyo timu hiyo inavyoweza kufanya vizuri bila ya kuwa na
wachezaji wa kigeni.
Si kwamba Mtibwa Sugar
haijawahi kusajili wachezaji wa kigeni, la hasha. Lakini ni nadra na hata
isipokuwa nao, basi inaendelea kufanya vema.
Msimu huu hadi Ligi Kuu Bara
inasimama, Mtibwa Sugar imepata sifa mbili kuu; kwanza kuwa timu inayoongoza
ligi hiyo, pili; ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza hata mchezo mmoja.
Usisahau Mtibwa Sugar haina
mchezaji hata mmoja wa kigeni, hali kadhalika haina hata kocha mmoja wa kigeni.
Ukiachana na hayo, kuna
mambo mengi wadau kama tukikubali kujifunza, tunaweza kuitumia Mtibwa Sugar
kama shule.
Kwani pamoja na kuwaamini
sana wachezaji wa kizalendo na bado ikaendelea kufanya vizuri, pia imekuwa
ikiwaamini makocha wazalendo tena wale wanaokulia katika mazingira ya timu
hiyo.
Unakumbuka wakati fulani
safu ya benchi lao la ufundi ilikuwa hivi; kocha mkuu, Mecky Maxime, msaidizi
wake, Zuberi Katwila na kocha wa makipa, Patrick Mwangata.
Hawa wote ni wazalendo
waliowahi kucheza katika kikosi cha Mtibwa Sugar na pia timu ya taifa, Taifa
Stars.
Wameaminiwa, timu yao
inafanya vizuri na wameweza kuifanya kazi yao hadi kuiondoa kabisa Mtibwa Sugar
kuwa kwenye kundi la timu zenye hofu ya kuteremka daraja.
Badala yake ni kati ya zile
zinazowania kuchukua ubingwa wa Tanzania Bara, nafasi ya pili au kubaki kwenye
kundi la kati, yaani hakuna presha ya kushuka au kuwa bingwa.
Kitu kizuri naweza kusema,
ikiwezekana wafanye kila linalowezekana wachukue ubingwa ili kuingia kwenye
kundi, hata wazalendo wana uwezo huo wa kuchukua ubingwa maana katika siku za
hivi karibuni, makocha wanaobeba ubingwa ni wale wa kigeni tu!
Kingine ambacho naweza
kusema ndiyo nilikilenga zaidi kwamba tunaweza kujifunza kupitia kwa Mtibwa
Sugar ni kuhusiana na wachezaji ambao huonekana hawafai kwenye klabu zao,
halafu Mtibwa Sugar inawachukua na wanafanya vema.
Hii si mara ya kwanza au ya
pili, Mtibwa Sugar imekuwa ikiwachukua wachezaji kutoka katika klabu mbalimbali
na hasa Yanga na Simba ambako walitoka wakionekana wamekwisha au wamepoteza
mwelekeo, halafu wanaanza kufanya vema.
Mfano wa karibu kwa msimu
huu ni David Luhende aliyetoka Yanga akionekana hana lolote au Mussa Hassan
Mgosi na Henry Joseph, wakongwe walioonekana ni kazi bure Simba, leo ndiyo
wanaozisumbua klabu zao za zamani zikikutana na Mtibwa Sugar!
Mtibwa Sugar inajua namna
ya ‘kujipikilisha’ na wakongwe hao hadi msosi unaiva vizuri na wanakuwa tishio
kwa waliowaona hawana kitu. Jiulize wanafanyaje?
Ukiachana na hivyo, pia
angalia Mtibwa Sugar walivyo na uwezo mkubwa wa kuwafufua wachezaji wenye
vipaji, wakawapa nafasi na baadaye kuwa kivutio kikubwa kwa wakongwe kama Yanga
na Simba au Azam FC.
Safari hii, Simba
imelazimisha hadi imefanikiwa kumpata beki wa kulia kutoka Mtibwa Sugar,
Ramadhani Kessy ambaye kabla hakuonekana kama ni lolote hadi timu hiyo ilipompa
nafasi.
Usisahau Amir Maftah wakati
akiwa beki bora wa kushoto nchini alitokea Mtibwa Sugar kwenda Yanga kama
ilivyokuwa kwa akina Victor Costa Nampoka na Mgosi pia ambao walijiunga na
Simba na baadaye kuwa lulu.
Lazima tukubali mfumo wa
Mtibwa Sugar ni bora. Tukikubali pia ni rahisi sana kujifunza na tunaweza
kubadilisha mambo kadhaa.
0 COMMENTS:
Post a Comment