MWAKA jana nilikuwa Mtanzania pekee
niliyeshiriki utoaji maoni, uundwaji na uendeshaji wa taasisi maarufu ya The 1
in 11 Campaign ambayo inashirikiana na klabu ya Barcelona na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Unicef kuhakikisha zaidi ya watoto milioni 30 wa bara la Asia
wasiokuwa na uwezi wa kifedha, wanakwenda shule.
Hakuna ubishi, katika dunia hii masikini
zaidi wako katika mabara matatu ya Afrika, Asia na Amerika Kusini. The 1 in 11
Campaign imewakomboa wengi sana barani Asia.
Nilichangia mambo kadhaa ya kimuundo na
kupewa majibu ya ahsante kutokana na nilikitengeneza kuwa ni msaada mkubwa.
Lakini nilihoji vipi hakuna kitu kama hicho barani Afrika? Bado sijapata jibu.
Huenda nikasubiri jibu kwa muda mrefu bila
ya mafanikio na hakuna njia lahisi ya kulazimisha hilo lifanyike. Bado macho na
moyo wangu kwa kushirikiana vinaona watoto wengi wa Kitanzania hawajaenda shule
licha ya kuwa na uwezo mkubwa kiakili darasani.
Wanashindwa kwenda kutokana na umasikini wa
familia zao. Au wana wazazi wenye uwezo lakini si wale wanaowajali vijana wao
na huenda pombe na ngono ndiyo wamezipa kipaumbele.
Nimepita katika mateso makubwa ya kukosa ada
nikiwa mdogo sababu ya mirafakano ya kifamilia. Kitu kinachoniumiza nikiona
Mtanzania mwenzangu pia ameshindwa kwenda shule sababu ya ada halafu bado
nikawa sina uwezo wa kumsaidia.
Ninaamini kabla ya kusubiri The 1 in 11
Campaign waje barani Afrika na baadaye kufika Tanzania, basi sisi wenyewe
tunaweza kujisaidia tukautumia mpira kama sehemu ya kuisaidia jamii na si
kusaidia kundi la watu wachache peke yao.
Soka kuchangia kwenye jamii ni jambo zuri
kwa kuwa ni mchezo wa jamii. Ndiyo maana Barcelona wanashiriki na balozi wao ni
nyota Lionel Messi.
Usiseme Simba, Yanga, Azam FC, Mtibwa Sugar
na wengine wanatafuta fedha hivyo hawawezi kuchangia elimu, itakuwa kichekesho.
Hata hapa nyumbani kuna tamasha la mara moja
kwa mwaka, linaitwa Tamasha la Matumaini, limekuwa likichangia elimu na tayari
kuna mabweni kibao yamejengwa kwa tamasha hilo.
Ndiyo maana nasema soka pia linaweza
kuchangia elimu, kusaidia watoto wa wasiokuwa na uwezo au watoto wenye uwezo
wasio na nafasi ya kwenda shule wakasome.
Mjadala wangu wa mapato ya mechi ya Nani
Mtani Jembe kati ya Simba dhidi ya Yanga nauendeleza hapa. Kwamba zile fedha
ambazo zimeyayuka kusikojulikana, basi zingeweza kusaidia kupeleka wadogo zetu
wengi wakasome shule.
Kuwa na taifa la watu wengi walioelimika ni
bora zaidi. Soka inaweza kusaidia, naendelea kuhoji zile fedha za Nani Mtani
Jembe ni nani na nani walichukua na iliwaje?
Kuna msomaji mmoja wa Championi kutoka
mkoani Morogoro ambaye alichangia kuhoji mapato hayo na ujumbe wake
ukachapishwa na gazeti hili alipiga simu na kulalamika alikuwa akitishiwa na
mtu aliyejitambulisha anatokea Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Nikalifuatilia hilo, lakini ilionekana
hakuna uhakika wa hilo na mimi nikamueleza inaonekana mtu yule hatokei TBL
huenda ana maslahi yake binafsi na anataka kulitumia vibaya jina hilo.
Lakini mimi bia kuna mtu alinipigia akihoji
kwamba TBL haijachukua fedha kwa nini ninaiweka kwenye mlolongo huo? Sasa
ninajua waandaaji walikuwa wao, halafu hatujui fedha zimekwenda wapi! Pia
sijawahi kusema TBL wamechukua, ila ninahoji na ninaona wao wanaweza
wakatueleza.
Fedha zilizopatikana kwenye Mtani Jembe,
Simba, Yanga, TFF na wadau wengine wangefaidika. Lakini ninaamini hata vijana
wa Kitanzania wangeweza kufaidika kielimu kama ambavyo The 1 in 11 Campaign
inasaidia barani Asia. Fedha za
Mtani Jembe zinaweza kuanza kusaidia na kama zimetumiwa tuambiwe ni kina nani!
0 COMMENTS:
Post a Comment