January 21, 2015


Na Saleh Ally
GUMZO la wiki hii katika michezo ni picha ya beki wa Ruvu Shooting, George Michael akimkaba kwa nguvu zake zote mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe raia wa Burundi.


Picha pekee mali ya gazeti hili, inaonyesha Tambwe akitokwa damu mdomoni wakati Michael akimkaba kwa nguvu bila ya huruma.

Muonekano wa picha hiyo umeonyesha kuwashitua wadau wengi wa soka kama ambavyo iliwashitua wahariri wa gazeti hili kwa mara ya kwanza walipoiona.

Haionyeshi uungwana, haionyeshi kama soka ni mchezo, inaonyesha soka ni vita au mchezo wa chuki na kulenga kuumizana.

Rekodi zinaonyesha katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara kati ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting msimu uliopita, Tambwe alifunga mabao matatu.


Mechi ya kwanza sare ya bao 1-1, Tambwe alifunga kwa penalti. Mechi ya pili, Michael alikuwa majeruhi, Simba ikashinda 3-2, Tambwe akifunga mabao mawili.

Maana yake hii ni mara ya tatu Tambwe anakutana na Ruvu Shooting hakufunga bao. Inawezekana Michael alifanikiwa kumzuia, lakini njia alizotumia, hakika si sahihi kimchezo.

Baada ya picha hiyo kutumiwa na Gazeti la Championi Jumatatu, mjadala mkubwa ulizuka katika vijiwe, kwa viongozi wa soka na wadau wengine mbalimbali. Wengi wamekuwa wakipinga.

Kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kama Facebook na Instagram kulikuwa na gumzo kubwa ingawa wako walitanguliza ushabiki wakidai hata wachezaji wa Ruvu Shooting waliumizwa siku hiyo.


Kwenye matangazo ya vipindi vya michezo hasa juzi, gumzo la picha hiyo lilikuwa kubwa zaidi na ilifikia hadi Mwenyekiti wa Chama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza), Mussa Kisoki kukemea tukio hilo akisisitiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanapaswa kuchukua hatua.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, kama ilivyo kawaida yake, alizungumza mengi kuhusu suala hilo, lakini mara nyingi alijikanganya.

Mfano, alisema hofu yake picha hizo zilikuwa ni za kutengenezwa, hasa alipozungumza na Redio ya E FM, alipozungumza na Redio One Stereo, akasema picha anazikubali, lakini anataka ushahidi wa video, halikadhalika Clouds FC, alisema hivyo.

Picha hiyo bora katika michezo tokea kuanza mwaka 2015, inatufunza mengi sana wadau wa soka na tukikubali, tutapiga hatua.

Moja:
Watanzania wengi hasa wadau wa soka si watu wa kukubali makosa. Mfano Masau ambaye anadiriki kusema picha hiyo ni ya kutengenezwa au vipi wachezaji wake nao walipigwa lakini haikuonekana.

Picha zilizopigwa ni nyingi, hiyo ni kati ya iliyoaminika ni bora zaidi na hilo limedhihirika. Championi ndilo gazeti bora zaidi la michezo nchini na linasomwa na watu wengi zaidi kuliko jingine kwa sasa, halina sababu ya kuweka vitu vya kutengeneza kwa nia ya kupotosha.

Masau ni kati ya wadau wetu, tunajua hakosi Championi na hata amewahi kufika kwenye chumba chetu cha habari kututembelea na kuona tunafanyaje kazi zetu.

Hivyo, kwa mara nyingine tunamkaribisha ili aje kuiona picha hiyo naye awe huru kuthibitisha na kuiambia jamii kama kweli iligushiwa au la, sisi tunachoweza kuthibitisha, picha hiyo ni sahihi na ilipigwa kwa ubora wa juu na ndiyo kiwango cha Championi.

Pili:
Ushabiki usiokuwa na msingi, wako ambao waliendelea kusema kwa kuwa Tambwe yuko Yanga, ndiyo maana Championi wametoa.

Si sahihi, Championi halina itikadi. Hata kama wafanyakazi wake wana timu zao, lakini hawauweki kwenye kazi.

Siku chache zilizopita, tulitoa picha za mwamuzi akipigwa huku anakimbizwa. Siku chache baadaye Mwanaspoti nao wakafuatia na kuendelea kudhibitisha ubaya wa kupiga waamuzi kama tulivyoanza.

Kwanza niwapongeze Mwanaspoti kwa kutuunga mkono kulaani vitendo hivyo vibaya vya kupiga uamuzi lakini ni sehemu ya uthibitisho kwa hatuungi mkono mtu kuonewa bila ya kujali anatokea timu ipi. Championi ni lako wewe msomaji.

Tatu:
Watu wa michezo hatupendani, hili limethibitishwa kuanzia uwanjani wakati Michael akimkaba Tambwe hadi kwa viongozi na wadau.

Aliyemkaba vile Tambwe unafikiri ana ndoto ya kucheza zaidi ya Ligi Kuu Bara? Wapi atacheza zaidi ya hapa Tanzania aachiwe kufanya alichokifanya? Kumfanyia vile Tambwe ni kuonyesha chuki, hakuna upendo.

Kiongozi kama Masau kutetea ni sehemu nyingi ya kuonyesha kiongozi anaweza kumtetea hata anayelenga kuua au kuumiza akisahau kesho pia inaweza kumtokea mchezaji wake.

Mashabiki, wanaangalia tu Tambwe anachezea wapi, hawajali aliumizwa vipi! Wakati akiwa Simba, Championi liliwahi kuandika pia akilalamika kuhusu beki huyo ambaye alipewa jina la ‘beki katili’.

Nne:
Waamuzi nao wana tatizo, siku kadhaa zimepita tumepiga kelele kuhusiana nao kupigwa kila wakati ambalo si jambo sahihi.

Wakati tunawatetea kuna kila sababu ya kuwa imara zaidi na kufanya kazi yao kwa ufasaha. Mechi kati ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting ilikuwa na taswira ya mechi ya ndondo.

Aliyesababisha ifikie pale ni mwamuzi Mohamed Teofili kutoka Morogoro na huenda alikuwa mwoga kwa kuwa anachezesha timu ya jeshi ambao wana sifa za kupiga waamuzi kama ngoma kipindi hiki.

Teofili hakuwa sahihi kwa kuwa hakupaswa kuwa mwoga. Anatakiwa kufuata sheria 17 za soka na kutenda haki.

Waamuzi wanatakiwa kuwa imara na kufanya kazi yao kwa ufasaha, kuchekacheka kama alivyofanya Teofili hakuwezi kuwa suluhisho.

Mwamuzi anapokuwa makini, lazima mchezo unakwenda vizuri. Bila ya kujali mchezaji wa Yanga au Ruvu Shooting ndiye aliyekosea. Mwamuzi alitakiwa kutokuwa mwoga na kuchukua hatua kwa wakosefu.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic