Kuendelea kukatwa makato makubwa imeelezwa ndiyo chanzo cha kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa, kudorora uwanjani.
Ngassa amekuwa kwenye
kiwango cha chini msimu huu ikiwa ni tofauti na misimu mingine yote
iliyotangulia.
Kiungo huyo, alitua
kuichezea timu hiyo kwenye msimu wa 2013/2014, kwa makubaliano ya kulipa fedha
shilingi milioni 45, ikiwa ni deni la shilingi milioni 30 pamoja na faini ya
milioni 15 za Simba ili aweze kuitumikia timu yake ya Yanga.
Ngassa alitakiwa kulipa
fedha hizo, baada ya kusaini mara mbili Simba na Yanga na kama angeshindwa,
basi angefungiwa kucheza soka na kulipishwa faini kutokana na kitendo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo cha
habari kutoka kwa rafiki wa karibu wa kiungo huyo, Ngassa ameshindwa kucheza
katika kiwango chake kutokana na viongozi wa Yanga kumsusia deni la shilingi
milioni 45 anazodaiwa na Simba.
Chanzo hicho kilisema kwa
makubaliano waliyokubaliana kila mwezi, kiungo huyo alitakiwa kukatwa shilingi
500,000 katika sehemu ya mshahara wake, lakini baadaye mambo yakabadilika akawa
anakatwa shilingi 1,000,000.
“Wengi wanahoji kiwango cha
Ngassa kimeshuka lakini hawajui sababu, hivi sasa hayupo vizuri,
amechanganyikiwa kisaikolojia kutokana na deni analodaiwa kususiwa na Yanga,
iliyoamua alipe mwenyewe badala ya klabu kumsaidia kama walivyokubaliana
alipotoka Simba.
“Katika makubaliano yao,
yeye alitakiwa kukatwa kiasi cha shilingi 500,000 kwa kila mwezi na klabu
imuongezee kiasi flani cha fedha kitakachokwenda kwenye deni alilokopa ili
ailipe Simba fedha zao walizokuwa wanamdai.
“Kutokana na kiasi hicho
cha fedha anachokatwa, anakosa kabisa fedha za matumizi yeye na familia yake kwa
kuwa anabakiza kiasi kidogo kwenye mshahara wake.
“Isitoshe hizo fedha
zenyewe anazokatwa hazionekani kuongezeka kwenye akaunti hiyo iliyofunguliwa
kwa ajili ya kulipia deni hilo la mkopo anaodaiwa, hiyo ndiyo sababu ya msingi
Ngassa anashindwa kucheza kwa kujituma ikiwemo kufunga mabao.”
Alipotafutwa Ngassa
kuzungumzia hilo alisema: “Hizo taarifa umezipata wapi? Ni kweli kabisa hizo
taarifa, kisaikolojia akili yangu haipo vizuri kutokana na deni ninalodaiwa,
ukiangalia kiasi cha fedha ninachokatwa kwa kila mwezi ni kikubwa ambacho
hatujakubaliana hivyo.
“Tulikubaliana kuwa klabu
inisaidie kulipa deni la mkopo niliouchukua ili niwalipe Simba kwa makubaliano
ya mimi kukatwa 500,000 lakini ninashangaa imekuwa tofauti, wananikata 1,000,000
katika mshahara wangu.
“Wamenikata kiasi hicho cha
fedha kwa mwaka mmoja, sasa wanaponikata kiasi hicho cha fedha mimi ninabaki na
kiwango kidogo cha fedha ambacho hakinitoshi kuendesha maisha yangu,” alisema
Ngassa ambaye taarifa zinadai analipwa mshahara wa Sh milioni 2.5 kwa mwezi.
0 COMMENTS:
Post a Comment