Ofisa Habari mwenye mbwembwe na majigambo
mengi wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, juzi aliishiwa ujanja na kujikuta
akikimbilia polisi baada ya kutishiwa kifo na mzee mmoja anayedaiwa kuwa ni kiongozi
wa Coastal Union aliyemtaja kwa jina moja la Kitendo.
Mkasa huo wa aina yake ulitokea juzi Jumamosi
wakati timu hiyo ilipokwenda kuuangalia uwanja watakaochezea mechi ya Ligi Kuu
Bara dhidi ya Coastal Union iliyotarajiwa kupigwa jana Jumapili kwenye uwanja
huo.
Masau ameiambia SALEHJEMBE kuwa mbali na kiongozi huyo kumtishia kifo, pia alimshambulia kwa matusi
makali ya nguoni ambayo ni aibu kuyasema mbele ya watu.
“Kama unavyojua kanuni za soka, timu ngeni
inatakiwa kufanyia mazoezi kwenye uwanja husika itakaoutumia kwa ajili ya
kuuzoea uwanja, lakini viongozi wa Coastal Union walituomba tukafanyie mazoezi
uwanja maalum waliotupa wakiomba kuutumia kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi
ya kombaini ya Mombasa.
“Kutokana na mahusiano mazuri tuliyonayo kati
yetu na Coastal Union tukaona tuwaachie wautumie na sisi tukaenda kuutumia huo
uwanja waliotupatia, lakini jioni baada ya mazoezi tukaona ni vyema
tukawapeleka wachezaji wetu wakautazame uwanja.
“Tulipofika kwenye Uwanja wa Mkwakwani
tuliotakiwa kuutumia, ndiyo akanyanyuka mzee huyo (Kitendo) aliyekuwa amekaa
jukwaani na kuanza kunitolea matusi ya nguoni na kunitishia kuniua kwa njia ya
upepo.
“Baada ya kunipa vitisho vile, nikanona ni
vyema niende nikatoe taarifa polisi, kwa sababu kitisho cha kumuua mtu siyo
kidogo, huyo mzee ndiye aliyeanzisha fujo za mwanzoni nilizofanyiwa hapa
Mkwakwani wakati tulipokuja kucheza na Mgambo.
“Hivyo, mara baada ya kutoka uwanjani hapo,
mimi na viongozi wangu tukaenda Kituo cha Polisi cha Chumbageni hapa Tanga kwa
ajili ya kwenda kuripoti, pia tukatoa taarifa kwenye Chama cha Soka Mkoa wa
Tanga na kwa viongozi wa Coastal Union,” alisema Masau.
0 COMMENTS:
Post a Comment