Tokea alivyoondoka Simba, kocha Mzambia, Patrick Phiri,
amekuwa akiichungulia Simba kwa mbali na juzi alitamka kuwa timu hiyo ina
nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na kikosi
kikali ilichonacho.
Hata hivyo, Phiri amesema kuwa ni lazima
wachezaji wapambane kutokana na upinzani mkali uliopo kutoka kwa Yanga na Mtibwa
Sugar.
Phiri bado hajapata timu ya kufundisha baada
ya kuachana na Simba kutokana na matokeo mabaya katika mechi nane za ligi kuu,
ambapo timu hiyo ilishinda mchezo mmoja, sare sita na kipigo kimoja. Nafasi
yake ilichukuliwa na Mserbia, Goran Kopunovic.
Phiri amesema anaipa Simba nafasi ya kutwaa ubingwa lakini akasisitiza ni lazima ‘wakaze’
buti kwani haiwezi kuwa rahisi kutokana na uwepo wa Yanga na Mtibwa ambazo pia
anasema zina nafasi ya kufanya hivyo.
“Ukiniuliza swali hilo nitakwambia timu
ninayoijua, Simba wana nafasi ya kuchukua ubigwa msimu huu, kutokana na aina ya
wachezaji ilionao. Lakini ni lazima wajitume zaidi maana kuna timu kama Yanga
hata pia hao Mtibwa Sugar wana nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa,” alisema
Phiri.
Simba ya Kopunovic imekuwa moto wa kuotea
mbali tangu achukue mikoba hiyo, ambapo umekuwa ni mwendo wa kugawa dozi,
wakiwa tayari wamefanya maajabu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo
waliondoka na ubingwa kwa kuizima Mtibwa Sugar katika changamoto za mikwaju ya
penalti.
0 COMMENTS:
Post a Comment