January 19, 2015


Na Saleh Ally
KATIKA mechi mbili zijazo za Ligi Kuu England, Southampton watacheza dhidi ya Crystal Palace halafu Swansea.


Huenda zitakuwa mechi nzuri sana kwako kuona ufundi wa hali ya juu wa kikosi cha Southampton ambacho sasa kimeng’ang’ania katika nafasi ya tatu.

Huenda usipate nafasi kwa kuwa Southampton si zile timu vigogo ambazo zingekuvutia kuangalia mechi zao, lakini huenda ina vitu ambavyo kwa vigogo hao huwezi kuviona.

Ukitaja timu tatu zinazohofiwa England, kwamba kila timu ikikutana nao inajua kweli kazi ipo, basi hauwezi kuiacha Southampton.

Chini ya kocha Ronald Koeman, Southampton imezidi kuwa tishio msimu huu kwa kila timu inayokutana nayo bila ya kujali ina sifa ya ukubwa au udogo.


Takwimu zinaonyesha Southampton ndiyo timu bora zaidi katika mechi tano zilizopita ambazo imeshinda nne na kutoka sare moja tu ya bao 1-1 dhidi ya Chelsea.

Ukitaka kujua kweli ni kikosi chenye nguvu, katika mechi hizo tano za mwisho za Ligi Kuu England, tatu ni dhidi ya vigogo, Chelsea, Arsenal na Manchester United.

Katika vigogo hao, Chelsea pekee ndiyo iliyobahatika kupata sare hiyo, Arsenal ilitandikwa 2-0, Man United ikapigwa nyumbani kwao kwa bao 1-0 na mwisho Southampton ikavunja rekodi ya kutoshinda Old Trafford kwa zaidi ya miaka 20.

Hii timu ina kina nani? Utaona wengi si watu maarufu sana. Kwa Afrika Mashariki na Kati unaweza kumzungumzia Mkenya, Victor Wanyama na Mzambia, Emmanuel Mayuka.

Tena waliobaki ni baada ya timu hiyo kuuza nyota wake zaidi ya watano lakini imesaka vipaji upya, sasa inaendelea kuchapa mwendo huku ikiwa tishio kabisa.

Southampton ndiyo timu inayoonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kushinda nyumbani na ugenini. Haina ushindi wa nyumbani pekee, hivyo kila upande unapokutana nao, umeishaongeza hofu.


Katika mechi dhidi ya Man United, kulikuwa na dalili zote kuwa Mashetani hao wangepoteza mchezo kwa kuwa walibanwa na kushindwa kuonyesha cheche kabisa na walipofungwa, ikawa safari.

Aina ya ulinzi wake unaonekana tatizo kwa timu nyingi kuitoboa ngome yake, ndiyo maana ndiyo timu bora zaidi hadi sasa kwamba wakikutangulia, nafasi ya kusawazisha ni ndogo sana kutokana na nidhamu kubwa waliyonayo katika safu ya ulinzi.

Sifa nyingine kubwa ni matumizi ya nafasi. Southampton ipo katika timu tatu bora ambazo ni Chelsea, Arsenal na yenyewe ambazo zinatumia nafasi nyingi zaidi baada ya kuzitengeneza.

Kwenye msimamo iko katika nafasi ya tatu nyuma ya Chelsea na Manchester City. Kuanzia nafasi ya nne kuna timu nne ambazo zimesajiliwa kwa fedha rundo lakini zimeshindwa kuishusha timu hiyo hadi sasa.

Nafasi ya nne ipo Manchester United, inafuatiwa na Tottenham, Arsenal na Liverpool. Unajua timu hizo zilivyotumia mamilioni ya fedha ukilinganisha na Southampton?

Wao kama ni kumkimbiza mwizi, basi ni kimyakimya tu, maana hawana umaarufu mkubwa sana, lakini wapo katikati ya kundi la timu tajiri na maarufu.

Southampton si timu iliyomwaga fedha nyingi katika usajili, lakini wameingia kwenye kundi la matajiri si kwa wingi wa fedha zao, badala yake ubora soka lao.

Unaweza kulihakikisha hilo kwa kukaa karibu kwenye runinga na kuangalia namna kikosi hicho cha Mholanzi Koeman kinavyocheza soka la hesabu na umakini wa hali ya juu kwa kutumia wachezaji wa bei chee.


Ubora wa Southampton unadhihirisha kuwa, fedha haziwezi kuwa kila kitu lakini ubongo na moyo kwa maana ya akili na nia ya dhati ya kufanya, vikishirikiana vema, basi hakuna linaloshindikana hata mbele ya wenye fedha nyingi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic