Huenda utakuwa ni mwaka wa neema kwa mshambuliaji Mbwana Samatta wa TP
Mazembe kwa kuwa timu nne za Ulaya zimeonyesha nia ya kumchukua.
Habari za uhakika zimelifikia gazeti hili kuwa, timu nne kati ya
hizo ambazo ni kutoka katika nchi za Ufaransa na Italia, zimeonyesha nia ya
kufanya kazi na mshambuliaji huyo Mtanzania.
“Kweli tunayajua majina ya timu nne, kumekuwa na mawasiliano kupitia
meneja wake Tanzania pamoja na uongozi wa TP Mazembe,” kilieleza chanzo kutoka
Ufaransa.
“Tusingependa kuanza kueleza kila kilichopo kwa sasa, lakini
tunaamini Samatta anaondoka Mazembe msimu huu.”
Baada ya taarifa hizo, juhudi zilifanyika kumpata
meneja wake, Jamal Kisongo ambaye alitoa ushirikiano.
“Kweli kuna timu zinamhitaji, kama nilivyokueleza awali Mbwana si
mtu wa kwenda kufanya majaribio, badala yake kujiunga na timu na kuanza kazi.
“Sasa kinachofanyika ni taratibu na nimekuwa na mawasiliano na
uongozi wa TP Mazembe, hivyo vuteni subira kidogo,” alisema Kisongo akionyesha
kujiamini kuhusiana na mchezaji wake huyo.
Samatta yupo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mapumziko na amekuwa
mchezaji tegemeo wa kikosi cha Mazembe.
Awali
ilielezwa, mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi, alikuwa akifanya juhudi
kuhakikisha Samatta anabaki Lubumbashi, DR Congo, lakini Kisongo amehakikisha
anakwenda mbele zaidi ili kupata mafanikio zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment