February 6, 2015


Na Saleh Ally
Nilikuwa kati ya wapenda soka waliopata nafasi ya kushuhudia mechi kati ya wenyeji Coastal Union dhidi ya wageni wao Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.


Ilikuwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya timu kongwe ambazo  kila moja ina rekodi ya kuwahi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

Hakika ilikuwa ni mechi kubwa kwa kuwa Yanga na Coastal Union ni kati ya timu za wananchi na zenye kiwango kikubwa cha mashabiki wanaoziunga mkono.

Ingawa siungi mkono, lakini utaona watu waliojitokeza, upinzani wao na hata wakafikia kugombana. Maana yake kila upande una watu wake, tena wa kutosha na wenye machungu kwa timu zao.

Swali langu, Watanzania bila ya kujali ni Tanga, Shinyanga, Mwanza au Kigoma wana mapenzi na timu zao tu na si soka ya Tanzania?

Nauliza hivyo kwa kuwa swali linatuhusu Watanzania wote wapenda mpira katika maeneo husika. Mfano, nizungumzie Tanga na aibu ya Uwanja wa Mkwakwani katika mechi hiyo ya Coastal Union dhidi ya Yanga.

Wakati tukiangalia mechi hiyo kwenye runinga kupitia Azam TV, wengi ambao si wapenda soka walikuwa wakiuliza maswali yanayokasirisha. Mojawapo ni hili: “Mbona uwanja una sura mbaya hivyo, hebu angalia Afcon, kweli hamuoni vibaya kuangalia mpira mbaya hivyo?”

Maswali hayo yalikuwa yanakera, jibu la kwanza ni kwamba muulizaji hakuwa akijua lolote kuhusu soka. Lakini swali lake lilikuwa limejaa ukweli mtupu.

Tangu mtu huyo alipouliza, muda mwingi niliangalia mpira ule nikiwa najiuliza maswali mengi sana, hasa nilipoona wachezaji wakikokota mpira.

Hakika ilikuwa hovyo kabisa, hali haikuwa nzuri na unaweza kusema ni aibu kwa taifa letu kuwa mipango mingi ya madai ya kuendeleza soka huwa ni hadithi za udanganyifu.

Mfano mzuri, msimu ujao, Uwanja wa Mkwakwani kwa msimu mmoja utachezewa mechi 45 kwa kuwa kila moja kuanzia Coastal Union, Mgambo FC na African Sports iliyopanda, zitacheza mechi 15.

Yanga, Simba, Azam FC, Mtibwa Sugar na nyingi, kila moja itashuka mara tatu katika Dimba la Mkwakwani. Dimba bovu kabisa na aibu kwa soka hapa kwetu nyumbani.

Katika mechi ya Coastal Union dhidi ya Yanga, ilionekana wazi watu walishindwa hata kukokota vizuri mpira kutokana na uwanja kujaa mabonde.

Tunataka soka liendelee, kuwe na mchezo wa kuvutia na timu zinapigana vikumbo kusajili wachezaji ghali wa kimataifa, lakini kwa uwanja kama huo wa Mkwakwani maendeleo yatapatikana vipi?

Ndiyo maana nikauliza, Watanzania wanapenda timu zao tu na si mpira wa Tanzania? Maana vipi Mkwakwani uwe uwanja mbovu kiasi hicho wakati kuna rundo la timu kwenye mkoa huo zinazoshiriki Ligi Kuu Bara?

Inakuwaje wanaomiliki uwanja huo, CCM, wanashindwa kutengeneza uwanja bora wa kuchezea? Vipi wananchi wa Tanga hawapigi kelele ili kusaidia mabadiliko kwa wahusika kubanwa hadi watengeneze uwanja?

Kelele nyingi ooh, Coastal ya kwetu, mara ooh siyo ya kwao! Mbona hamsemi uwanja wenu ni aibu? Au hao wahusika mbona hawapambani kuondoa aibu hiyo kwa kutengeneza uwanja bora wa kuchezea wakati wakijua wana uwanja mbovu kabisa?

Kwa mechi 45 za msimu ujao ndani ya Mkwakwani, ni hadithi mpya inayoendelea kuwa ya Alinacha na kamwe mafanikio hayatapatikana.

Uwanja wa Mkwakwani katika eneo la kuchezea ni moja ya aibu za mpira wa Tanzania kwa kuwa pamoja na ukongwe wake, utaona Kambarage Shinyanga au Nangwanda Mtwara, ni viwanja bora na wahusika wanajua kwamba kweli ili kucheza soka bora, lakini uwe na uwanja bora.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic