Uongozi wa Klabu ya Yanga kupitia kwa
Mkurugenzi wa Sheria wa Yanga, Frank Chacha umesema unaendelea kumsubiri
mshambuliaji Geilson Santos Santana ‘Jaja’ raia wa Brazil aje nchini kuitikia
wito wa kesi waliyomfungulia.
Yanga ilimfungulia kesi mchezaji huyo Mahakama
ya Kazi Ilala ambapo imepangwa kusikilizwa Februari 16, ambapo Yanga inadai
mchezaji huyo alikiuka vifungu vya sheria wakati alipovunja mkataba wake na
timu hiyo.
Wakili Chacha amesema hawatafanya chochote kwa
kuwa kisheria mtuhumiwa bado ana nafasi tatu za kuitwa.
“Kwa mujibu wa sheria, ikitokea Jaja hakutokea
mahakamani wala kufanya lolote, basi kuna nafasi nyingine tatu za kumwita.
Tumeshamtumia e_mail, EMS na kumtumia balozi wake kwa ajili ya kuhakikisha ujumbe
wa wito unamfikia kwa wakati ili aweze kuja kusikiliza kesi yake,” alisema.
Yanga iliamua kumfungulia kesi hiyo Jaja
aliyejiunga na klabu hiyo Julai 12, 2014 kwa mkataba wa miaka miwili na inamdai
faini ya dola milioni mbili (Sh bilioni 3.2), fedha ya usajili dola 20,000 (Sh
milioni 32) na dola 3,000 za mshahara wake kwa mwezi mara miezi 12 (jumla Sh
milioni 57.6).








0 COMMENTS:
Post a Comment