Straika wa Yanga, Amissi Tambwe, ndiye gumzo
hivi sasa katika soka la Tanzania baada ya mabao yake mawili kuipa timu yake
ushindi wa 2-0 dhidi ya BDF XI lakini kitu kikubwa ni kwamba, muda mfupi tu
baada ya kuwaua Waswana hao, klabu yake imempatia nyumba.
Tambwe alifanikiwa kufunga mabao hayo katika mchezo
wa Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na wakati
mashabiki wakitoka uwanjani walikuwa wakiimba: Tambwe, Tambwe, Tambwe…”
Mrundi huyo ambaye ni mfungaji bora wa Ligi
Kuu Bara msimu uliopita (alipachika mabao 19), aliachwa na Simba katika usajili
wa Desemba, mwaka jana na juzi ndiyo alianza kuwaonyesha Yanga kwamba yeye ni
nani katika suala la kuzifumania nyavu kutokana na mabao yake kuwapa ushindi.
Mabao hayo aliyofunga Tambwe, yamesababisha
aweke rekodi ya kufunga mabao yote manne msimu huu kwa kutumia kichwa.
Bao lake la kwanza msimu huu alilifunga akiwa na
Simba kwenye mzunguko wa kwanza katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal
Union, baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa na Emmanuel Okwi
dakika ya 36.
Bao lake la pili alilifunga akiwa na Yanga
katika mzunguko wa pili kwenye sare tena ya mabao 2-2 dhidi ya Azam baada ya
kuunganisha kwa kichwa krosi ya Salum Telela, kabla ya juzi kuweka tena kambani
mabao mawili kwa vichwa katika mchezo dhidi ya BDF dakika ya kwanza na ya 55,
akiunganisha krosi za Haruna Niyonzima na Mrisho Ngassa.
Tambwe
amesema amefurahi kufikisha mabao matatu akiwa na Yanga lakini akatamba kwamba
ataendelea kufunga zaidi kama Mungu akiendelea kumpa afya.
“Naamini
nitaendelea kufanya vizuri zaidi. Hiyo ndiyo kiu yangu kubwa, nataka niwape
furaha mashabiki wa Yanga.
“Mungu anazidi kuwaonyesha Simba kwamba
walikuwa wanafiki kwa tuhuma walizokuwa wakinipatia,” alisema Tambwe.
“Tangu nijiunge na Yanga nilikuwa nikijisikia
vibaya kwa sababu nilikuwa sifungi hali hiyo pia ilinifanya nijione ni mwenye
deni kubwa sana kwa klabu yangu hii ambayo hakika naweza kusema inanijali sana.
“Hata hivyo namshuru sana Mungu kwa kusikia
kilio changu na kunifanya niisaidie timu yangu kuibuka na ushindi wa mabao 2-0,
hakika nimefarijika sana na najiona kama nimezaliwa upya.
“Nawashukuru pia wachezaji wenzangu wote kwa
ushirikiano wao mkubwa wanaouonyesha kwangu, siku zote na katika mechi ya leo
(juzi).”
Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga nao
umemzawadia Tambwe zawadi ya nyumba mpya ya kuishi kwa kipindi chote atakachokuwa
akiitumikia klabu hiyo kutokana na kuwezesha kuibuka na ushindi dhidi ya BDF
XI.
Nyumba hiyo ipo Sinza Mori jijini Dar es
Salaam na nyota huyo ambaye kwa sasa anaiishi Mabibo jijini hapa, anatarajia
kuhamia Jumatano hii.







0 COMMENTS:
Post a Comment