Timu ya Coastal Union ya Tanga imesema kuwa itahakikisha
inapambana vilivyo ili kuweza kuhakikisha inachukua pointi tatu muhimu dhidi ya
Mbeya City kwenye mechi ya Ligi kuu soka Tanzania Bara itakayochezwa wikiendi
hii kwenye uwanja wa Mkwakwani.
Coastal Union itangia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya
kupoteza mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa kwenye uwanja wa sokoine
jijini Mbeya ambapo Mbeya City iliweza kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ambalo
lilipatikana kwa njia ya penati.
Ofisa Habari wa
Coastal Union, Oscar Assenga amesema kuwa maandalizi ya kuelekea mechi hiyo
imekamilika kwa asilimia kubwa kwa kufanya mazoezi asubuhi na jioni.
Amesema kuwa mipango yake mikubwa ni kuhakikisha wanafuta
machungu ya kufungwa na Yanga bao 1-0, kwenye mechi yao ya Ligi kuu iliyochezwa
kwenye uwanja wao wa nyumbani jambo ambalo halikuwafurahisha mashabiki na
wapenzi wa soka.
Aidha amesema kutokana na kikosi chake kuendelea kuimarika kila
mchezo wanaokuwa wakicheza wana matumaini makubwa ya kupata ushindi ambao
utawawezesha kusogea kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi hiyo.
Alisema kuwa ligi kuu msimu huu imekuwa ni ngumu sana lakini kubwa ni
kujipanga hivyo wamejipanga vizuri kwa umakini mkubwa lengo likiwa kukiwezesha
kikosi hicho kinapata matokeo mazuri







0 COMMENTS:
Post a Comment