Chama cha kandanda mkoa wa Dar
es salaam DRFA,kimeeleza kusikitishwa kwake na kifo cha kiungo wa
zamani wa klabu ya Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Christopher Alex Massawe kilichotokea leo (februari 22 mwaka huu) katika
Hospitali ya Mirembe Dodoma.
Mwenyekiti wa DRFA,Almas
Kasongo,amemuelezea marehemu Christopher kuwa ni mchezaji aliyevuma enzi za
uhai wake na kuiletea heshima kubwa klabu yake ya Simba na Taifa Kwa
ujumla,pale walipofanikiwa kuisukumiza nje ya michuano ya afrika klabu ya
Zamalek na kuivua ubingwa miamba hiyo ya soka ya kaskazini mwaka 2003.
Kiungo huyo aliyeanza kuvuma
katika miaka ya 2000,amefariki dunia kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na
ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Marehemu Christopher Alex,
alizaliwa Septemba 12 mwaka 1975,na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya
msingi Uhuru na kumaliza katika shule ya Chamwino huko Dodoma mwaka 1993,na
alianza kucheza mpira kwenye timu ya Daraja la nne Chamwino UTD na baadaye
daraja la tatu akiwa na kikosi cha Aston Villa nayo ya Dodoma.
Mwaka 1999-2001 ameitumikia
klabu ya CDA ya Dodoma,kabla ya kutimkia klabu ya Reli mwaka 2002 na baadaye
kujiunga na wekundu wa msimbazi Simba,Marehemu ameacha mtoto mmoja aitwaye
Alex.
Kasongo, kwa niaba ya kamati ya
utendaji ya DRFA,wametoa ubani wa shilingi laki mbili (200,000/=) kwa familia
ya marehemu,na kuwataka mashabiki wa soka na watanzania kwa ujumla kuungana
pamoja katika kuifariji familia hiyo kwenye kipindi hiki kigumu cha majonzi.
0 COMMENTS:
Post a Comment