February 23, 2015


Na Saleh Ally
BAADA ya soka, mchezo wa ngumi ndiyo wenye mashabiki wengi zaidi nchini. Inawezekana hii ikawa kwingine kote duniani ingawa nchi nyingine zina aina nyingi ya michezo iliyo hai.


Hakuna ubishi kuthibitishwa kwa pambano la wakali wawili wa mchezo wa ngumi duniani Floyd Maywether dhidi ya Manny Pacquiao ni mtikisiko wa maswali mengi yasiyokuwa na majibu hadi hapo itakapowadia Mei 2, mwaka huu kwenye Ukumbi wa MGM Grand jijini Los Angeles, Marekani.

Wawili hao wamekubali kupanda ulingoni katika pambano hilo linalochukua historia ya kuwa pambano la kufunga midomo na ghali zaidi katika mchezo wa ngumi kwa kuwa litagharimu zaidi ya dola milioni 250 (Sh bilioni 425).

Kati ya fedha hizo, Mayweather atachukua dola milioni 150 (zaidi ya Sh bilioni 255) huku Pacquiao kutoka Ufilipino akiondoka na dola milioni 100 (zaidi ya Sh bilioni 170).


Pambano hilo limekuwa katika mjadala kwa miaka mitano sasa, huku kila mmoja akionyesha kuwa na hofu na mwenzake.

Wakati fulani, ilifikia Pacquiao ambaye ni mbunge kukubali kucheza lakini akagoma kutekeleza pendekezo la Maywether kumtaka apimwe kama hutumia dawa za kuongeza nguvu au la.

Kukataa kwa Pacquiao, kulifanya pambano hilo liendelee kuwa hadithi kwa muda huo lakini sasa kinachosubiriwa ni ndondi na si vinginevyo kwa kuwa Pacquiao amekubali kupimwa, kitu ambacho awali aliona ni kama kudhalilishwa.


Kila mmoja amekuwa akitamba kivyake lakini ukweli au jibu sahihi ni Mei 2 kwenye Ukumbi wa MGM Grand Garden Arena. Pambano hilo ni ghali zaidi kutokea katika mchezo wa ngumi na mara tu baada ya mabondia hao kusaini mkataba huo, fedha zimeanza kumiminika.

Makampuni mawili maarufu ya runinga, maarufu katika kuonyesha mchezo wa ngumi ya HBO na Showtime, yamekubali kutoa mamilioni ya fedha kuonyesha pambano hilo.

Nini kinachovuta?
Wengi wanajiuliza ni kipi hasa kinachowachanganya wengi? Mabondia hao ndiyo bora zaidi katika kizazi cha sasa ulingoni.

Hakuna aliyetarajia siku moja wangekutana katika ulingo mmoja. Baada ya chenga za miaka mitano, sasa wanakutana na ubishi utamalizwa.

Rekodi zao pia ni chanzo kikuu, Mayweather (47-0, 26 KO). Hajapoteza hata pambano moja katika hayo 47 na ameshinda 26 kwa KO huku akitamba Pacquiao atakuwa mtu wa 48 kumchapa.


Kwa Pacquiao rekodi ni (57-5-2, 38 KO). Utaona Mfilipino huyo ameishapoteza mapambano matano na sare mbili, lakini bado haitishi kumshusha.

Pacquiao amecheza mechi nyingi zaidi ya Maywether, ana sare nyingi zaidi, ameshinda nyingi zaidi hali kadhalika ana idadi kubwa zaidi ya sare na kupoteza.

Aina ya upiganaji:
Hii ni sehemu ya pili kwa ukubwa inayowavutia wengi kuona wawili hao wanapigana tena. Kasi yao, mbinu na vipawa vya hali ya juu katika upiganaji.

Mayweather anaaminika ndiye bondia mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kujilinda dhidi ya wengine wote duniani, lakini Pacquiao ndiye anayesifika kwa kutegua mitego mingi zaidi, hapo ndiyo patamu.

Haukujua hili:
Kesho Jumanne, Mayweather anatimiza miaka 38, hivyo atacheza pambano hilo akiwa anamzidi Paquiao miaka miwili, kwa kuwa ana 36.

Kikubwa zaidi ambacho haukujua, promota aliyemtoa Mayweather aitwaye Bob Arum, sasa ndiye promota wa Pacquiao baada ya kukorofishana na bondia huyo mwaka 2006.

Mayweather alianza kucheza ngumi za kulipwa mwaka 1996 baada ya kung’ara katika Olimpiki, akachukuliwa na Bob Arum kabla ya kukorofishana miaka 10 baadaye. Hivyo ushindani ndani hadi nye ya ulingo ni mkubwa.

Tiketi:
Umeambiwa ni pambano ghali, hivyo lazima tiketi ziwe ghali na kweli ‘hazishikiki’.

Tiketi ya bei rahisi imeelezwa kuwa dola 5,000 (Sh milioni 8.5) wakati zile zinazozunguka ulingo zimepaa hadi kufikia dola 26,500 (zaidi ya Sh milioni 45), kama unaishi Bongo, chagua ukaone pambano hilo ‘live’ au ununue Toyota IST zako tano zote ufanye teksi!


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic