Shirikisho
la Mpira wa Miguu nchini (TFF) jana limefanya Mkutano Mkuu wa Mwaka katika
ukumbi wa Morogoro hoteli ya mjini Morogoro ambapo mgeni Rasmi alikua ni mkuu
wa mkoa wa Morogoro Dr Rajabu Rutengwe.
Katika
hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo, Dr Rutengwe aliushukuru uongozi wa TFF
nchini kwa kuweza kuandaa mkutano mkuu mzuri na wa kisasa ambao pia ulifanyikia
katika mkoa wake wa Morogoro.
Akiongea na
wajumbe wa mkutano mkuu Dr Rutengwe alisema, TFF ina changamoto ambazo inapaswa
kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wa mpira wa miguu nchini kwa ujumla,
changamoto hizo ni kukosekana kwa wataalamu wa vyakula, wataalamu wa tiba na
wataalamu wa saikolojia.
Dr Rutengwe
aliomba TFF kwa kushirikiana na serikali inapaswa kuandaa wataalamu wengi wa
masuala hayo ili kuweza kuendana na mahitaji ya kuwaanda wanamichezo bora ambao
watakua tayari kwa ushindani na sio ushiriki.
Aidha mkuu
wa mkoa huyo aliipongeza Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuupa mkoa wa Morogoro
uenyeji wa mkutano mkuu ambapo pia umefanyika na malengo kufanikiwa kwa
asilimia mia moja, na kusema kwa niaba ya serikali ya mkoa wapo tayari kupokea
tena mwaliko wa uenyeji wa mikutano mbalimbali ya TFF.
Mkutano
ulijadili Ajenda za kawaida ambazo ni Kufungua Mkutano ni Uhakiki wa Wajumbe, Kuthibitisha
Muhtsari wa Mkutano Mkuu uliopita, Yatokanayo na Mkutano uliopita, Hotuba ya
Rais, ripoti kutoka kwa Wanachama, Kuthibitisha ripoti ya utekelezaji wa
Kamati ya Utendaji.
Zingine ni
Kuthibitisha ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013, Kuthibitisha ripoti ya Kamati ya
Ukaguzi wa Hesabu, Kupitisha bajeti ya 2015, Marekebisho ya
Katiba, Mengineyo na Kufunga Mkutano.
Kwa mara
ya kwanza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limepata bendera yake ambayo
ilipitishwa na mkutano mkuu na asubuhi ya jumapili Machi 15 mwaka huu,
imepandishwa kwa mara ya kwanza Morogoro hoteli.
Aidha
wajumbe wa mkutano mkuu pia wamepitisha azimio la kuanzishwa kwa mfuko wa
maendeleo ya mpira wa miguu nchini (FDF), ambapo kutaundwa kamisheni maalum
itakayoshugulikia suala hilo.
Lengo la
kamisheni hiyo ni kuisaidia TFF kuandaa na kuratibu mipango ya maendeleo ya
soka la watoto, vijana, wanawake nchini na kuviwezesha vyama vya soka vya mikoa
(FA), vyama shiriki vya TFF kujiendesha katika shughuli mbalimbali za maendeleo
ya soka la vijana.
Pia
mkutano mkuu huo ulitoa azimio la kuitaka serikali itoe msamaha wa kodi kwa
vifaa vya michezo hasa vinavyotumika kufundishia watoto michezo.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na wajumbe 125 na kati yao wajumbe watano ni wanawake.
Kikao
kijacho cha mkutano mkuu kitafanyika kati ya mwezi Novemba na Disemba mwaka huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment