Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, ametamka kwa kujiamini
kuwa, kama uongozi wao utafanya usajili kwa wachezaji waliowapendekeza kwenye
ripoti, hakika timu za ligi kuu zitakiona cha moto.
Mkwasa ambaye anafanya kazi chini ya Mholanzi, Hans van Der Pluijm,
amesema walipendekeza wachezaji bora sana na anaamini kuwa wakipatikana wote
basi watafanya vizuri kwenye ligi ambayo ina timu bora kama Simba, Azam na
Mbeya City.
Kauli hiyo, ameitoa ikiwa ni siku chache tangu viongozi wa timu
hiyo wafanikishe usajili wa kiungo mshambuliaji wa Mbeya City, Deus Kaseke
aliyesaini mkataba wa miaka miwili.
Mkwasa alisema kuwa ripoti waliyoikabidhi kwa viongozi inaeleza
kuwa wamelenga kufanya usajili bora wa kushiriki vyema Ligi ya Mabingwa Afrika
na siyo ligi kuu tu ili kuhakikisha timu inafikia malengo.
“Kama tuliweza kufanya
vizuri kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Afrika tulilotolewa na Etoile du
Sahel, mwaka huu kwa kikosi kile tulichokuwa nacho, itashindikana vipi
tushindwe kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa tutakayoshiriki mwakani.
“Ninaamini katika michuano ya kimataifa ya mwakani tutafanya
vizuri, tena katika kiwango kikubwa kutokana na ripoti ya usajili
tuliyoikabidhi benchi la ufundi kwa viongozi wa kamati husika.
“Tumepanga kusajili wachezaji watakaotufikisha katika ‘levo’ za
kimataifa, nawapongeza viongozi kwa kufanikisha usajili wa Kaseke ambaye yeye
alikuwepo kwenye orodha ya wachezaji tuliowapendekeza,” alisema Mkwasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment