MAKINDA: AJIBU KULIA NA MAKAPU WAMEITWA KATIKA KIKOSI CHA TAIFA STARS |
Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya
Tanzania 'Taifa Stars', Mart Nooij leo ametangaza kikosi cha wachezaji 28
watakaoingia kambini katika hoteli ya Tansoma iliyo eneo la Gerezani jijini Dar
es salaam, kujiandaa na michuano ya kombe la COSAFA na kuwania kufuzu kwa AFCON
na CHAN mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amesema wachezaji 28 aliowaita, amewaona kwa macho yake wakicheza, na katika wachezaji
aliowaita amechanganya wanaochipukia (damu changa) na wenye uzoefu wa michuano
ya kimataifa.
Nooij amesema katika orodha
hiyo ya wachezaji 28 watakaoripoti kambini jumatatu mchana, watapimwa afya zao
na madakatari wa timu ya Taifa, na kisha watakaokuwa fit atachagua wachezaji 20
watakaokwenda kwenye michuano ya COSAFA nchini Afrika kusini.
Aidha Nooij ameongeza
wachezaji 8 watakaobakia nchini wanapaswa kuwa tayari wakati wowote wanaweza
jumuishwa katika kikosi kutokana na Taifa Stars kukabiliwa na michuano
mbalimbali ambayo pia inahitaji kuwa na wigo mpana wa wachezaji.
Wachezaji walioitwa na kocha
Nooij ni magolikipa: Deogratius Munish (Yanga), Aishi Manula, Mwadini Ali
(Azam), walinzi: Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam), Nadir
Haroub, Oscar Joshua, Kelvin Yondani (Yanga), Abdi Banda, Hassan Isihaka
(Simba), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Haji Mwinyi (KMKM).
Wengine ni viungo: Amri
Kiemba, Salum Abubakar, Frank Domayo (Azam), Said Juma 'Makapu', Salum Telela, Hassan
Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba), Haroun Chanongo (Stand United) na Mwinyi
Kazimoto (Al Markhiya).
Washambuliaji ni Ibrahim Ajibu (Simba), Mrisho Ngasa, Simon Msuva (Yanga), John Bocco, Kelvin Friday (Azam)
na Juma Luizio (Zesco United).
Taifa Stars inatarajiwa
kuondoka nchini siku ya jumatano, Mei 13 saa 1 jioni kwa shirika la ndege la
Fastjet kuelekea nchini Afrika Kusini katika mji wa Rusterburg - North West
Province ambapo ndipo michuano ya COSAFA CUP itafanyika kuanzia Mei 17 mpaka
Mei 31 mwaka huu.
Mchezo wa kwanza wa Taifa
Stars iliyopo katika kundi B katika michuano ya COSAFA, itacheza dhidi ya
Swaziland Mei 18, Mei 20 (Madagascar Vs Tanzania) na Mei 22 ( Tanzania vs
Lesotho), mshindi wa kundi B atacheza robo fainali dhidi ya timu ya Taifa
kutoka Ghana.
Mara baada ya kumalizika kwa
michuano hiyo, Taifa Stars itarejea nchini kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu
kwa AFCON 2017, dhidi ya Misri utakaopigwa Juni 13 nchini Misri, kisha kurejea
nchini kucheza na Uganda Juni 21 kuwania kufuzu kwa fainali za wachezaji wa
ndani CHAN.
Mart Nooij amesema ataitumia
michuano ya COSAFA kama sehemu ya maandalizi ya michezo ya kuwania kufuzu kwa
AFCON na CHAN.
IMETOLEWA NA MSEMAJI WA TFF, BARAKA KIZUGUTO
0 COMMENTS:
Post a Comment