Winga Ramadhan Singano ‘Messi’
anapingana na Simba kuhusu uhalali wa muda wa mkataba wake na kuna uwezekano
ukawa mwisho wa mkataba wake kuitumikia timu hiyo.
Hata hivyo, anaweza kujifariji kwani
Azam FC imesema inafuatilia kwa kila hatua malumbano hayo na yakiisha tu
itamsajili Messi ili kuongeza nguvu katika safu yake ya ushambuliaji.
Kwa siku tatu sasa, Messi amekuwa
akisisitiza anamaliza mkataba wake wa miaka miwili kuitumikia Simba aliosaini
mwaka juzi, lakini Simba inasisitiza bado mwaka mmoja katika mkataba wake kwani
alisaini miaka mitatu.
Messi akasisitiza kuwa kuna wajanja
waliobadili vipengele vya mkataba wake uliopelekwa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), ndipo Azam ilipojitanua na kusema; “Messi maliza matatizo yako uje
usaini mkataba huku.”
Katibu Mkuu wa Azam, Idrisa Nassor
alisema: “Tunamtaka Messi amalize matatizo yake na Simba halafu aje tuzungumze
naye halafu tukikubaliana tumsajili.”
Nassor alisema Messi ni aina ya
wachezaji wanaowahitaji kwa ajili ya kuwasajili katika kukiimarisha kikosi chao
katika kuelekea michuano ya kimataifa itakayoshiriki ambayo ni Kombe la
Shirikisho na Kombe la Kagame.
“Wakati tukionyesha nia ya kumsajili,
tumetoa masharti yafuatayo, kwanza kabisa kumaliza matatizo ya kimkataba kati
yake na uongozi wa Simba.
“Kama akimalizana nao, basi sisi tutakaa
naye meza moja kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumsainisha mkataba wa
kuichezea Azam,” alisema Nassoro huku habari za ndani zikieleza kuwa timu hiyo
imeachana na kiungo Amri Kiemba aliyekuwa akiichezea kwa mkopo.
0 COMMENTS:
Post a Comment