Na Saleh Ally
MIAKA 26 ya uhai
wake, Steven George Gerrard ameimalizia akiwa katika klabu moja tu ya
Liverpool, hiki si kitu kidogo.
Gerrard alijiunga na
Liverpool akiwa na umri wa miaka minane tu, baada ya mkuza vipaji mmoja
kumuona. Ameichezea timu kubwa ya Liverpool kwa miaka 17, tena kwa mafanikio
makubwa ambayo hayana mfano.
Leo Gerrard anaondoka
Liverpool kwenda kujiunga na LA Galaxy ya Marekani kwa mkataba wa dola milioni
9 (Sh Bilioni 18), fedha ambazo soka ya Tanzania ambayo inakua kwa mwendo wa
kinyonga haijawahi kupata mchezaji aliyeuzwa hata robo ya fedha hizo.
Gerrard anaondoka
Liverpool akiwa na miaka 34. Anauzwa kwa thamani ambayo hazina Yanga wala Simba.
Hakuna mchezaji kijana au mzee wa Tanzania mwenye robo ya thamani hiyo.
Kujituma kwa aina
gani? Nidhamu ya juu kwa kiasi kikubwa ambayo nani anaweza kuwa nayo? Gerrard
anamshangaza kila mmoja, lakini nani angeweza kufanya kama yeye?
Liverpool ndiyo klabu
ya kwanza ya England kuwa na mashabiki wengi nchini
humo. Gerrard ndiye mchezaji aliyezungumzwa zaidi
kwa kipindi kirefu kuliko wengine wote hapa Tanzania.
Ameshinda makombe
muhimu 10 akiwa na Liverpool kama utazungumzia Kombe la FA, lile la Ligi, Ligi
ya Mabingwa Ulaya na mengineyo.
Akiwa nahodha wa
Liverpool ameshinda zaidi ya zawadi binafsi 20. Ubora wa Gerrard unawezekana
kwa hapa nyumbani Tanzania?
Wangapi wamedumu kwa
muda mrefu katika klabu zetu? Wangapi wamekuwa tayari kujitolea kwa dhati hadi
kufikia mafanikio makubwa kwa siku nyingi!
Unaweza kusema
Gerrard alikuwa katika mazingira mazuri na Liverpool, ndiyo maana amedumu sana.
Lakini utakuwa hujawahi kusikia matatizo makubwa yaliyomkuta akiwa na klabu
hiyo, lakini akabaki hadi kufikisha miaka 17 akiwa na timu kubwa.
Unakumbuka mashabiki
walivyomshambulia mama yake mzazi kwa maneno makali ya kumdhalilisha? Wakati
fulani, mashabiki walichoma moto jezi yake akishuhudia kwenye runinga! Bado
Liverpool ilimzungusha kumsajili kwa kiasi kikubwa siku chache baada ya kuipa
ubingwa wa Ulaya kule Istambul, Uturuki.
Wakati huo Chelsea
chini ya Jose Mourinho ilikuwa tayari kumchukua kwa kitita kikubwa. Lakini
akavumilia hadi mwisho na kuchukua kiasi cha kawaida na kubaki tena Liverpool?
Si lazima mchezaji
Mtanzania aone haiwezekani lakini si vizuri kumuacha Gerrard aondoke bila
yeyote kujifunza kuhusiana naye. Mtu aliyepitia mengi ya kukatisha tamaa, lakini
akayashinda na juzi ameagwa kama shujaa.
Mabao 503 katika
mechi 119 kwa kiungo si kitu kidogo. Huyu anaonyesha hakuwa mtu mzembe, hakuwa
mtu wa kulaumu tu, mtu wa kulia anaonewa huku akiwa hajitumi kufanya lolote.
Rekodi za Gerrard
zilijengwa na hali ya kutaka kushinda. Hali ya kupambana bila kuchoka na nia ya
kushinda kila wakati bila ya woga.
Ambacho amekikosa
katika maisha yake ya soka ni Kombe la Ligi Kuu England. Lakini kila mmoja
ataona alivyokuwa akipambana hadi siku ya mwisho, katika maisha bahati mbaya
ipo.
Tafuta mchezaji sasa
anayeweza kufanana hata kidogo na Gerrard. Lakini vipi mchezaji fulani anataka
kujifananisha naye ndotoni bila ya kuiga aliyokuwa akiyafanya.
Nahodha anayeaminika
hata wakiteuliwa manahodha wengine 11 kuunda kikosi maarufu duniani, basi yeye
atakuwa nahodha wao anakwenda ‘kupumzika’ Marekani na kumalizia soka lake.
Gerrard ni ubao wa
darasani ambao tayari una maandishi maalum ambayo unaweza kuwafunza wachezaji
wengi wa Tanzania kwamba kuna mengi aliyoyafanya yeye yanawezekana.
Mazingira ni jambo
moja, si rahisi mchezaji wa Tanzania akataka kufanikiwa kwa mazingira ya
England. Lakini anaweza kumtumia Gerrard kama mfano na vizuri kuangalia maisha
ya ndani na nje ya uwanja pia.
Akiwa kinda, kweli
amewahi kuingia katika misukosuko kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufikishwa
mahakamani. Lakini alipofunga ndoa na Alex Curran, baadaye wakafanikiwa kupata
mabinti watatu, Lilly-Ella, Lexie na Lourdes alionyesha tofauti kubwa na
alisifia namna mkewe alivyokuwa akimuunga mkono.
Familia ikishirikishwa,
inaweza kuwa msaada. Huenda familia za Kitanzania au Kiafrika zinaweza
kujifunza kwamba kama zitamuunga mkono mhusika wao, anaweza kufanikiwa.
Gerrard ni kamanda.
Kweli anakwenda lakini lazima tukubali kwamba si sahihi kumuacha akaenda bila
kumtumia kama funzo kubwa angalau kwa machache tu.
Mvuto wa ushabiki,
sawa. Lakini mvuto wa mafunzo kupitia yeye ni mkubwa zaidi na anaweza kusaidia.
MAKOMBE:
KOMBE LA FA
2001, 2006
KOMBE LA LIGI
2001,2003, 2012
NGAO YA JAMII:
2006
LIGI YA MABINGWA
2005
KOMBE LA UEFA
2001
UEFA Super Cup
2001, 2005
0 COMMENTS:
Post a Comment