Na Saleh Ally
TAARIFA zinazohusiana na usajili wa
msimu mpya wa 2015-16, ndizo zimetawala kila sehemu, hasa vyombo vya habari.
Kila timu inajitahidi kujiimarisha na
jambo la kwanza ni kusajili wachezaji bora kabisa, hakuna anayetaka mambo ya
kubahatisha.
Ubaya wa usajili, mara zote huwa hauna
uhakika wa asilimia mia, maana unayemsajili naye ni binadamu. Anaweza kufanya
vizuri au akaboronga na kukuingiza matatizoni.
AJIBU. |
Lakini kama kunakuwa na umakini, basi
suala la kutokea hofu ya kubahatisha linakuwa dogo pia kwa kuwa wanaofanya
hivyo wanakuwa wanakwenda katika kitu sahihi.
Wachezaji wamekuwa wakitaka fedha
nyingi, mfano mzuri ni Malimi Busungu, amewaambia Simba anataka Sh milioni 40,
mimi nikajiuliza za nini sasa?
Sifa nzuri ya mshambuliaji ni kufunga
mabao. Akiwa na Mgambo FC, Busungu amefunga mabao 9. Najiuliza mabao hayo
yanatosha kwake kuona ana thamani ya Sh milioni 40? Ningekuwa najijibu,
ningesema hapana.
Inawezekana ningekubali kumuongezea
mshahara wake hata mara tatu au nne. Hasa kama analipwa Sh 400,000 au chini ya
hapo. Lakini lazima tukubaliane, washambuliaji wengi Watanzania wamefeli,
lazima wakubaliane na hilo.
Tathmini nzuri ni Ligi Kuu Bara msimu
uliopita kwa kuwa ukiangalia tano bora ya wafungaji, kinara ni Mtanzania, Simon
Msuva aliyefunga mabao 17. Baada ya hapo hutapata Mtanzania!
Wa pili ni Amissi Tambwe wa Yanga,
raia wa Burundi mwenye mabao 14, anafuatiwa na Mnigeria anayecheza Stand
United, Abasrim Chidiebere ambaye ana 11, Emmanuel Okwi wa Simba kutoka Uganda
ana 10, sawa na Didier Kavumbagu wa Burundi.
Hata ukisema kumuingiza Rashid Mandawa
wa Kagera Sugar, basi lazima agombee nafasi kati yake na Kavumbagu na Okwi.
Lengo si kulaumu, lakini kutoa
changamoto kwamba wachezaji wengi wa Kitanzania hawana mwendo bora katika kazi
zao.
Mfano mzuri ni wafungaji bora wa miaka
miwili au mitatu, Mrisho Ngassa wa Yanga na John Bocco, wameporomoka kabisa. Msimu
uliopita, Ngassa amemaliza akiwa na mabao manne tu na Bocco ana mawili tu,
anaweza kusema majeraha, lakini tumo humohumo.
Angalia Ame Ali wa Mtibwa Sugar, alianza
mzunguko wa kwanza vizuri sana, akionekana tishio, lakini amemaliza akiwa na
mabao 9. Ilionekana angemaliza ligi akiwa na 23 au zaidi lakini wapi.
Tambwe ambaye alikuwa mfungaji bora
msimu mmoja nyuma kwa mabao yake 19, aliondoka Simba msimu uliopita tena akiwa
ameshaifungia bao moja. Amejiunga Yanga katikati, timu ambayo hajaizoea, kapiga
13. Sasa ameshika nafasi ya pili.
Msimu mmoja alikuwa mfungaji bora, tena
ukiwa wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara. Uliofuata akashika nafasi ya pili,
utaona kuwa huyu ni mshambuliaji wa aina yake kabisa!
Watanzania wanashindwa nini? Aliyetamba
msimu uliopita, atakuwa hovyo kabisa msimu ujao, wanasumbuliwa na ugonjwa gani?
Kuvimba vichwa? Kujisahau? Au nini?
Ukweli ni kuwa wamefeli msimu uliopita,
tena wengine wakajitangaza majina wakitaka walipwe mamilioni hata yasiyo ya
uwezo wao kitu ambacho ni tatizo kubwa.
Kuna kila sababu ya kuangalia msimu
ujao.
Maana washambuliaji wengi wa Tanzania
wamefeli katika ligi yao ya nyumbani, sehemu pekee ambayo wangeweza kujidai
angalau, maana Tanzania haina wachezaji wengi wa kulipwa!
Nyumbani hawapo, wageni wanatamba.
Ugenini hawapo kwa kuwa hawawezi kutamba, sasa wanaweza kutamba wapi hawa
washambuliaji wa Kitanzania? Lazima watafakari.
Hata wasifiwe vipi, bado haukuwa msimu
mzuri kwao kwa kuwa hata mfungaji bora mwenyewe, hakuwa na mabao mengi. Ni
chini ya 20, tena chini ya wafungaji bora wa misimu mitatu nyuma. Hivyo kama
ingekuwa ni simu wanapiga, basi wrong number. Wajaribu tena msimu ujao.
Akina Serrunkuma wamelipwa sh ngapi na wamefanya nini!!? Tuache kubeza vya nyumbani!! Kama Okwi na Niyonzima wanachukua zaidi ya mill 80, kwa nini leo Busungu asipate hata nusu yake
ReplyDelete