Mtibwa Sugar wala haina
kinyongo na sasa ipo katika mchakato wa kuwarejesha wachezaji wake walioachwa
na Simba na Yanga ili waanze upya harakati zao za soka.
Muda wowote kuanzia sasa
Mtibwa ya Turiani, Morogoro itakuwa imeshawarejesha beki wa kushoto Issa Rashid
‘Baba Ubaya’ kutoka Simba na straika Said Bahanuzi kutoka Yanga. Pia imepanga
kumsajili Haruna Chanongo aliyemaliza mkataba Simba.
Kwa mujibu wa habari
kutoka ndani ya klabu hiyo, wachezaji hao wameshafanya mazungumzo ya awali na
klabu hiyo na muda wowote kuanzia sasa watasaini mikataba yao.
“Wala hatuna matatizo na
hao wachezaji kwani waliondoka kwa heshima na tunawarejesha baada ya mambo yao
kukwama, tutahakikisha tunamalizana nao muda wowote na hata huyo Chanongo
tutamsajili,” kilisema chanzo chetu.
Alipotafutwa Ofisa Habari
wa Mtibwa, Thobias Kifaru alisema; “Kwa sasa hatujafanya usajili wowote, zaidi
tunasubiri bodi ya timu ikutane kujadiliana ishu ya usajili na mambo ya kocha.”
Mtibwa ipo katika
mchakato wa kumpa kazi Kocha Piet De Mol kutoka Ubelgiji kuchukua nafasi ya
Mecky Maxime ambaye tayari ameanza kazi Taifa Stars kama kocha msaidizi.
0 COMMENTS:
Post a Comment