Pamoja na kumsaini winga , Deus Kaseke na straika
Malimi Busungu, bado Yanga wamesema hawajaridhika zaidi, hivyo wanataka
kuongeza nguvu kwenye wingi zote- kulia na kushoto.
Katika kufanikisha hilo, Kocha Mkuu, Hans van Der Pluijm,
anatarajiwa kushuka Bongo ndani ya wiki hii ambapo ataambatana na wachezaji
wawili wanaomudu wingi ya kulia na kushoto.
Habari kutoka Yanga zinasema kuwa lilikuwa pendekezo la kocha
mwenyewe, lakini taarifa nzuri kwa Wanayanga ni kwamba nyota hao ni kama
mapacha- wanajuana kwa kina, kwani wote wanatokea timu moja inayoshiriki ligi
kuu nchini Ghana.
Taarifa hizo zimekwenda mbali na kufafanua kuwa mbali na Ghana,
pia mitego imetegwa katika nchi nyingine tano ambazo ni Rwanda, Benin, Sierra
Leone, Zimbambwe na Nigeria.
Nafasi ambazo zinatolewa macho zaidi ni beki wa kulia ambaye anategwa
nchini Benin, huku nchi nyingine wakiangalia zaidi kuimarisha safu ya
ushambuliaji na kiungo wa kati.
“Tumeamua kuangalia zaidi kuimarisha winga zetu, ukiangalia
Coutinho hana msaidizi kama ilivyo kwa Kaseke. Na wote atakuja nao kocha
akitoka kwenye mapumziko huko Ghana, sijawajua majina ila wanatoka timu moja,”
kilisema chanzo hicho.
Katibu wa klabu hiyo, Dk Jonas Tiboroha, amesema mpango wa kusaka wachezaji wa kimataifa, lakini kikwazo ni
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchelewa kutoa msimamo wao juu ya ombi la
kutaka idadi ya wachezaji wa kigeni kuongezeka kutoka watano hadi nane.
“Ni kweli kuna wachezaji wa kigeni tunawafuatilia kwa karibu
lakini kama unavyojua tayari tumejaza nafasi za wageni, kwa sasa tunasubiri
tamko la TFF ili tuangalie cha kufanya zaidi, lakini kuhusu ujio wa kocha na
wachezaji hajaniambia,” alisema Dk Tiboroha.
0 COMMENTS:
Post a Comment