July 18, 2015


Na Saleh Ally
KOCHA wa Manchester United, Louis van Gaal, amechukua uamuzi wa moja kwa moja kumtimua kipa Victor Valdes baada ya kukiuka agizo lake la kutaka akacheze katika timu za vijana.


Valdes kaonyesha ni mkubwa na jeuri, lakini van Gaal kaonyesha ni mkubwa zaidi yake, mwisho uamuzi unafuatia, mshindi lazima atakuwa kocha huyo.

Kocha Hans van Der Pluijm ndiye alitoa uamuzi wa mwisho wa kuachwa kwa kiungo aliyeitwa kipenzi cha Wanayanga, Athumani Iddi ‘Chuji’. Wapo walioona alikuwa anakosea, wakasogea kumsihi na hata viongozi wakajaribu kumshawishi ampe muda.

Msimamo wa Pluijm ukawa ni uleule, Chuji akaondoka Yanga. Leo kuna waliopata nafasi yake wanaonekana, jiulize nani angemuona vizuri Frank Domayo au Salum Telela lakini sasa Said Juma ‘Makapu’?
 
PLUIJM
Kocha Mfaransa Patrick Liewig, mara tu maada ya Simba kurejea kutoka Oman, akatoa msimamo wake kwamba wakongwe kadhaa, akiwemo Haruna Moshi ‘Boban’, kipenzi cha Wanasimba hawapaswi kuendelea kuichezea Simba.

Boban alikuwa ‘roho’ ya Wanasimba, lakini Liewig akashikilia msimamo wake, akatoa nafasi kwa vijana wakiwemo ambao baadaye walikuja kuwa hazina ya Simba hadi leo hii. Boban akaondoka zake na Simba imeendelea na maisha yake na watu wamesahau.

Kocha Alex Ferguson alipata mafanikio makubwa sana katika kipindi chake cha zaidi ya miaka 20 akiwa na Manchester United. Lakini ukisoma kitabu chake au wale waliokifuatilia kupitia gazeti hili, watakuwa wamejifunza mambo mengi sana.
 
FERGUSON
Kwamba Ferguson amepitia milima na mabonde na ugumu wa kazi yake haukuwa kwa mashabiki zaidi, badala yake wachezaji ambao alilazimika kupambana nao kweli.

Mfano kuondoka kwa David Beckham, Roy Keane ambaye hadi leo haelewani naye. Utaona lilikuwa ni suala la kushikilia msimamo wake kama kocha kwa manufaa ya timu kwa kuwa Keane alikuwa akionyesha dharau ya wazi kwa msaidizi wake, Carlos Quieroz akitaka ampande kichwani.

Kawaida, wachezaji wanapofanikiwa na kuwa maarufu huwa wana mafariki wawili wakubwa. Viongozi wa klabu na mashabiki ambao huwa wanawatetea kwa kila namna kuhakikisha ikiwezekana hata kocha afanye anavyotaka mchezaji.

Ferguson anasema kwa kocha yeyote akiteleza na mchezaji mmoja au wawili wakawa juu ya kichwa cha kocha, basi ajue amekwisha!

Amekwisha kwa kuwa kazi itamshinda. Ferguson anaamini kocha anatakiwa kuwa juu ya wachezaji wote, bila ya kujali umaarufu au utajiri wao. Kocha ndiye mhimili, mzazi na kiongozi wa timu.

Mchezaji anabaki kuwa sehemu au mtoto ndani ya timu. Mfano mzuri katika familia zetu za Kiswahili, mtoto mwenye uwezo kifedha anaweza kusikilizwa na wazazi hadi kufikia kuingiza chuki au dharau. Hapa mzazi anapaswa kusimamia muongozo sahihi bila ya kujali nani ana uwezo upi.
 
LIEWIG
Unaweza kusema misimamo ya Pluijm na Liewig ndiyo iliyowang’oa Chuji na Boban katika vikosi vya Simba na Yanga. Hakika angekuwa Boniface Mkwasa au Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, wasingeweza maana kama wangeitwa na viongozi au kupigiwa simu na mashabiki maarufu, basi wangeshindwa kushikilia msimamo wao.

Kilichowafanya makocha hao kuwaondoa wachezaji hao ilikuwa ni nidhamu na hakuna jambo jingine. Hawaonyeshi kujituma, lakini muonekano wa kawaida kwamba wao ni nyota hivyo hawaguswi.

Ukiangalia hayo ndiyo mambo wanayofanya akina Ferguson, van Gaal, Arsene Wenger na wengine wengi, jambo ambalo hata makocha wazalendo wanapaswa kujifunza.

Kuna wakati unafikia unakiamini kitu, lakini inakuwa vigumu sana kuwashawishi watu mapema. Ukichukua uamuzi wa kukifanya unaweza kujikuta umebaki peke yako au na watu wachache sana wanaokuunga mkono.

Kama ni muoga utaachia njiani, lakini kama uko thabiti, basi hutayumba na kuhofia maneno na haya ndiyo wanayofanya makocha wengi wenye mafanikio kama ulivyoona Jose Mourinho wa Chelsea alipoamua kuwatosa wachezaji nyota kama Juan Mata na David Luiz kwa kukubali kuwauza halafu bado timu yake ikawa bingwa wa England.

Lakini makocha wazawa wakubali kwamba kama wana uwezo, kujiamini na kuchukua maamuzi magumu ambayo hata kama si sahihi leo, yanaweza kuwa sahihi baadaye, basi nayo ni sehemu ya ubora wa uwezo sahihi na ndiyo moja ya vitu wanavyokosa, wachukue sasa ili kujiimarisha zaidi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic