Na Saleh Ally
LEO ni fainali ya 44 ya michuano ya Bara la Amerika Kusini maarufu
kama Copa America na gumzo kubwa ni Lionel Messi maarufu kama Leo.
Messi au Leo kama anavyoitwa na wachezaji wenzake na mashabiki
wengi wa Hispania, ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Argentina, mchezaji ambaye
amekuwa akionekana hana bahati akiwa na kikosi cha timu yake ya taifa.
Pamoja na kuwa bora kuliko mchezaji mwingine katika sayari ya dunia,
lakini Messi hajawahi kubeba ubingwa wa Copa Amerika wala Kombe la Dunia akiwa
na Argentina.
Mafanikio makubwa akiwa na Barcelona ambayo ameiongoza kuchukua
kila ubingwa unaotambulika duniani kwa ngazi ya klabu, yamegeuzwa kuwa fimbo ya
kumchapia.
Kwamba hana msaada kwa taifa lake kama ambavyo amekuwa akitoa
msaada katika timu yake ya Barcelona ambayo ilimlea kisoka tangu akiwa na miaka
13.
2007:
Akiwa na umri wa miaka 20, Messi aliteuliwa kuwa mchezaji bora
kijana wa michuano hiyo.
Katika mechi ya kwanza,
alitoa pasi safi kwa Herman Crespo wakati Argentina ikiitwanga Marekani 4-1.
Mechi iliyofuata dhidi ya Colombia, akaangushwa na kusababisha penalti,
wakashinda 4-2. Katika mechi ya tatu dhidi ya Paraguay, Messi akatoa pasi
nyingine kwa Javier Mascherano.
Katika robo fainali, Argentina ikaishinda Peru bao 4-0, pia
akafunga bao. Bao la pili akafunga wakati wa mechi ya nusu fainali wakiishinda
Mexico 3-0.
Mechi ya fainali, Argentina wakakutana na kipondo cha mabao 3-0
kutoka kwa Brazil waliokuwa mabingwa.
2011:
Alikuwa ndiyo ameteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Dunia 2010,
Argentina wakawa wenyeji wa michuano na matumaini makubwa.
Akiwa amefunga mabao 12 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia
kuisaidia Barcelona kushinda ubingwa wa tatu katika miaka sita, bado hakuweza
kuisaidia Argentina kuwa bingwa.
Messi alimaliza akiwa ametoa asisti nyingi zaidi, alitoa 3.
Argentina wakang’olewa kwenye robo fainali kwa mikwaju ya penalti dhidi ya
Uruguay.
2015:
Kwa Messi, hii imekuwa michuano ya tatu ya Copa America ambayo
Argentina imeingia fainali dhidi ya wenyeji Chile ambao tayari wameonyesha
uwezo mkubwa sana.
Utaona kikubwa leo ni ndoto kati ya wenyeji dhidi ya Messi
anayetajwa dunia nzima na huenda mashabiki wake wakiwemo wale ambao hata si
raia wa Argentina, wangependa kuona anaondoa ‘ugwadu’ huo wa kushindwa kubeba
makombe akiwa na Argentina.
Safari yake inaonekana imekuwa ni kupanda juu ingawa gumzo ni
kwamba msimu huu ameonekana hana mabao zaidi ya lile moja tu alilofunga mwanzo.
Lakini ana pasi tatu za mabao, achana na hivyo, katika ushindi wa
mabao 6-1 iliouopata Argentina dhidi ya Paraguay na kutinga fainali, Messi
alikuwa chanzo kwa kutengeneza mabao matano kwa kuwa chanzo cha mipango.
Chile wako vizuri, lakini kwa hali ilivyo na kiwango cha Messi cha
mechi mbili zilizopita za Copa America, inaonekana hazuiliki.
Chile ambao watakuwa nyumbani wakitaka kuwaonyesha wananchi wao
kuwa ni kikosi cha mwaka wa dhahabu kwa kuwa wameingia fainali baada ya kuikosa
kwa zaidi ya miaka 20, lazima ukumbuke, wanalitaka kombe hilo huenda kuliko Messi.
Wachezaji kama Arturo Vidal na Alexis Sanchez nao watakuwa na njaa
ya mafanikio na heshima leo, lakini wanaweza vipi kumzuia Messi aliye katika
msitu wa mafundi kama Angel Di Maria, Sergio Aguero na wengine kibao?
Asilimia hadi 70 kwa Argentina kuwa mabingwa, 30 tuwaachie Chile.
Lakini unaporudi katika suala la soka, bado lazima utoe nafasi ya 50-50 kwa
kuwa ni mchezo ambao hauna matokeo ya moja kwa moja kwa kuwa hautabiriki.
Maana yake, Messi anapaswa kusubiri hadi mwisho wa dakika 90 ili
kujua kama ameweza kuondoa ‘nuski’ ya kushindwa kufanya vema akiwa na Argentina
kwa kubeba ubingwa huo.
Kwa miaka kibao sasa, huenda mechi hiyo ya fainali ya Copa America
leo, itakuwa ni ile iliyobeba hisia zaidi kuliko nyingine zote kwa kuwa Messi
na wenyeji ni kati ya wenye hisia kali ya ushindi na kulibeba kombe lakini
lazima mpira uchezwe hadi kipenga cha mwisho ili jibu lipatikane.
Ukiangalia rekodi za tangu 2007, inaonekana Messi amekuwa akipanda
na kushuka. Walifika fainali mwaka huo yeye akiwa kinda, mara ya pili
wakadondoka robo fainali na sasa wako fainali.
Ni zamu ya Messi? Lazima usubiri na kushuhudia mchezo utakavyokuwa
ili kupata jibu sahihi.
MESSI NA COPA AMERICA:
MICHUANO
MABAO ASISTI MECHI NAFASI
2007 2 1 6 Namba 2
2011
0 3 4 Robo fainali
2015
1 3 5 Fainali
0 COMMENTS:
Post a Comment