July 4, 2015

 
BIN SLUM AKIWA NA MWANAYE ABDULWAHAB...
NA SALEH ALLY
SIKU iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na Coastal Union, imewadia, ni kesho Jumapili.


Klabu hiyo kubwa nchini baada ya Yanga na Simba itakuwa inafanya uchaguzi wa viongozi wake baada ya kupita katika vipindi vigumu vya mfarakano, kutengana kabla ya kurekebishana.

Mmoja wa wadau wakubwa wa Coastal Union ni Nassor Bin Slum ambaye ni shabiki wa kugaragara na mwanachama wa kitambo wa Coastal Union.

Bin Slum alipotafutwa na gazeti hili kwa ajili ya kutoa maoni yake kuhusiana na uchaguzi wa kesho ambao utakuwa dira mpya kwa klabu hiyo, akalishangaza gazeti hili baada ya kusema hatapiga kura.


Championi: Hautashiriki uchaguzi, umesusa?
Bin Slum: (Tabasamu) Umeenda mbali sana. Coastal ni klabu yangu, sijasusa. Ninasafiri na familia, sitakuwepo nchini.

Championi: Ok, sasa nini labda ungewashauri wanachama wenzako wakifanye katika uchaguzi wa kesho ambao ni dira mpya ya klabu?
Bin Slum: Hakika nina mengi, kwanza wasiuchukulie uchaguzi kama fasheni au kukomoana lakini uwe kama sehemu ya siku sahihi ya kuwavusha kutoka katika matatizo.

Championi: Unaposema fasheni unamaanisha nini?
Bin Slum: Lengo langu si kumpigia yeyote kampeni lakini watu wasichague kwa kuangalia ndugu au rafiki zao, wasiwakate wale wenye uwezo kwa kuwa si ndugu au rafiki zao. Waangalie maslahi ya Coastal Union.

Championi: Unafikiri bado kuna wale wanaokumbuka yaliyopita kwa maana ya kutoelewana?
Bin Slum: Ndiyo, inawezekana lakini lazima tusahau na kuangalia nini cha kufanya kupata Coastal Union mpya.


Championi: Unafikiri wachague viongozi wa aina gani wenye sifa sahihi ya kuikomboa Coastal Union?
Bin Slum: Viongozi wenye nia ya kusaidia Coastal Union, wanaojua umuhimu wa nidhamu, wanaokubali kukosolewa kwa ajili ya kuijenga klabu ila wawe wanaoamini umoja wa Wanacoastal ni dawa na nguvu ya kuleta maendeleo.

Pia wawe watakaoipa ubingwa wa Tanzania Bara ndani ya kipindi chao cha miaka minne. Si kugombea kuepuka kuteremka daraja tu. Ushindi wa timu ni sehemu ya morali ya ubora ndani ya klabu.

Championi: Unafikiri viongozi waliopita hawakuwa wakikubali kukosolewa?
Bin Slum: Wako waliokuwa hivyo, lakini hiyo ni sehemu ya matatizo makubwa yaliyotuangusha. Lazima tubadilike.

Championi: Kuna taarifa zinasema, viongozi wasioamini ushirikina hawapewi nafasi Coastal Union?
Bin Slum: Kuhusu kutopewa nafasi sijui, lakini suala la ushirikina eti timu ishindwe limepitwa na wakati. Lazima tuwe na viongozi imara watakaoibadili Coastal Union na kuwa ya karne hii inayotaka kubeba ubingwa si kuamini ushirikina.

Championi: Unafikiri katika wagombea mtapata wanaoweza kuiondoa Coastal kuwa tegemezi?
Bin Slum: Wapo, ninaamini wanaoweza kuikwamua Coastal Union ni Wanacoastal wenyewe ndiyo maana nasisitiza wachague watu sahihi kwa maslahi ya klabu.

Championi: Kila baada ya uchaguzi, kumekuwa na makundi, lililoshinda na lililoshindwa, unafikiri Coastal wanaweza kuliepuka hilo?
Bin Slum: Hakika inawezekana, Coastal wanaweza kuliondoa hilo kwa kuwa hiki si chama cha siasa ambacho umesikia kuna makundi na wakati mwingine watu wanahama.

Hauwezi kuhama klabu, isipokuwa mashabiki na wanachama wachache wendawazimu ambao tumewahi kuwasikia.

Championi: Baada ya uchaguzi, nini kifanyike kuua hayo makundi?
Bin Slum: Baada ya uchaguzi kitu cha kwanza ni kuvunja makundi. Uongozi uliopita ulifeli, ulikuwa wa kwanza kuanzisha makundi na kuwatenga wanachama na mashabiki. Watakaoingia wajue sumu iliyowaangusha waliopita, hivyo Coastal iwe moja baada ya uchaguzi.

Championi: Unafikiri makundi yatavunjwa kama wagombea walioshindwa hawatakubali kushindwa?
Bin Slum: Hakika itakuwa vigumu, lakini lazima wakubali ili kurudisha Coastal Union moja. Walioshinda, nao wanaweza kuwa sehemu ya kuvunja makundi kwa kuwaita waliowashinda na kuwaunganisha kuisaidia klabu.

Walioshindwa bado wanabaki kuwa Coastal, hivyo wawaingize kwenye baadhi ya kamati na wao watoe mchango wao katika maendeleo ya klabu.

Championi: Umekuwa mdhamini, mkurugenzi wa ufundi kabla ya kujitoa. Je, baada ya uongozi mpya kuingia madarakani, uko tayari kushirikiana na uongozi mpya?


Bin Slum: Mimi ni Coastal Union, inategemea watakuja vipi, tutajadili nini. Sitaweza kurudi kama zamani hadi kuwa kiongozi. Kusaidiana ni jambo bora na kuhakikisha Coastal inakuwa timu ya kugombea ubingwa. Kikubwa hapa ni Coastal Union kwanza, mtu baadaye.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic