![]() |
| SAMATTA... |
Klabu ya kongwe
barani Afrika, Zamalek ya Misri imetoa kitita cha dola milioni 1 (zaidi ya Sh
bilioni 2) kumsajili mshambuliaji Mtanzania, Mbwana Samatta anayekipiga TP
Mazembe.
Samatta
anayekipiga katika kikosi hicho cha matajiri wa DR Congo, anaweka rekodi ya
kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania, kupewa dili kubwa kama hilo la kununuliwa.
Tokea mchezo wa
soka nchini uanzishwe, Samatta anayelamba dola 10,000 (zaidi ya Sh milioni 20)
kwa mwezi, ndiye amefikia thamani ya mchezaji anayeweza kununuliwa kwa Sh zaidi
ya bilioni moja.
Mwenyekiti wa
Zamalek, Mourtada Mansour ameliamchia Championi Jumatatu katika mahojiano
maalum kutoka Misri kwamba, wametoa kitita hicho cha dola milioni moja, ili
wamnase Samatta na kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.
Lakini akasema
amekuwa na masikitiko makubwa baada ya kuambiwa Samatta amekataa kwenda kucheza
Misri kwa kuwa asingependa kubaki Afrika tena.
“Kweli, tumetoa
fedha hizo. Tunaamini hiyo ni thamani ya Samatta, tumempa heshima yake. Lakini
bado inaonekana hataki tena kucheza Afrika baada ya kuondoka Mazembe. Huenda
tutajaribu tena,” alisema Mansour.
“Bado tunaendelea
kumshawishi, kama anataka kwenda Ulaya, hapa Zamalek ni lahisi kuonekana.
Unawakumbuka akina Junior Agogo, Amri Zakh, Emanuel Amuneke, Mido na wengine
wengi walitokea hapa.”
Taarifa hizo za
kwamba Samatta amekataa fedha hizo, zilishitua gazeti hili ambalo lilifanya
juhudi za kumpata kwa siku tatu lakini bila ya mafanikio.
Siku ya tano,
Samatta alipatikana, safari hii akiwa nchini Morocco ambako TP Mazembe imeweka
kambi kujiandaa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, pia ligi ya DR Congo.
“Ni kweli, Zamalek
waliwasiliana na wakala na meneja wangu. Walitoa hiyo dola milioni moja, lakini bado nina mipango mingine,”
alisema Samatta.
“Ningependa kutoka
nje ya Afrika baada ya TP Mazembe. Hivyo ninaendelea kupambana kufikia
ninachohitaji,” alisema Samatta akisisitiza anamuachia Mungu huku yeye
akiendelea kujituma kwa juhudi kuu.
Samatta ni kati ya
wachezaji waliocheza Ligi Kuu Bara kwa muda mchache sana lakini wana mafanikio
makubwa sasa. Katika ligi hiyo aliichezea Simba akitokea Mbagala Market ambayo
ilibadili jina na kuwa African Lyon baada ya kununuliwa na milione, Mohammed
Dewji aliyekubali atue Simba wakati akiiuza.
SOURCE: CHAMPIONI








0 COMMENTS:
Post a Comment