Na Saleh Ally
NIMEKUWA wazi kila mara kuhusiana
na mwenendo wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa),
kwamba linakwenda kwa kubahatisha.
Nimekuwa nikieleza namna baraza
hilo linavyokuwa kama mali ya kundi dogo tu la watu ambalo linaongozwa na
Katibu Mkuu, Nicholas Musonye.
Musonye, raia wa Kenya, amekuwa
akiiongoza Cecafa kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Yupo tu hapo na baraza
linaendelea kuwa lilelile.
Ndani ya Cacafa hakuna mabadiliko
makubwa ukiachana na viongozi wachache ambao wamekuwa wakichaguliwa kama ilivyo
kwa sasa, rais ni Leodegar Tenga aliyewahi kuliongoza Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF).
Pamoja na kuwepo kwa rais kutoka
nchi tofauti lakini inaonekana wazi mtendaji mkuu ambaye ni katibu mkuu,
amekuwa akiiendesha Cecafa kwa mwendo uleule.
Mara kadhaa, nimekuwa
nikipinga kwamba uendeshaji wa mambo ya Cecafa hadi yanafikia kuwa ni ya
upendeleo wa aina fulani kama ambavyo unapoona michuano inachezwa Rwanda, basi
kuna haki fulani ya kutaka kumridhisha mdhamini mkuu, Rais Paul Kagame wa nchi
hiyo.
Sina shida na Kagame, inawezekana
hawezi kuwa na muda wa kutaka timu za pale nyumbani zipendelewe lakini Cecafa
wanalazimika ‘kujigonga’.
Kanuni za uendeshaji michuano yake
na hasa inapofikia hatua za klabu, nimekuwa nikiona zimejaa ubabaishaji mkubwa
wa mambo na moja ya mfano ni ile makala niliyoiandika Jumatatu kuhusiana na
Metodo.
Kwamba wakati hapa nyumbani
michuano ya Kagame inazidi kushika kasi, timu zinazoshiriki zikiwemo tatu za
Tanzania, zimeonekana bure kwenye runinga. Kama ni hivyo, fedha za udhamini
kutoka katika runinga ya SuperSport, zimekwenda wapi?
Cecafa wanalalamika
kuhusiana na kutokuwa na fedha. Utaona Gor Mahia kutoka Kenya ilikuwa
inakaribia kujitoa hadi ilipopewa fedha na Serikali ya Kenya, ndiyo ikaondoka
kuja kushiriki.
Cecafa haiwezi kulipa nauli ya
timu, haiwezi kulipa malazi ya zaidi ya wachezaji 20. Mamilioni kutoka
SuperSport yanakwenda wapi?
Angalia Azam TV inatoa Sh milioni
100 kwa msimu mmoja. Angalau tungeambiwa timu zinalipwa hata kama ni Sh milioni
20 au zaidi kwa kuwa SuperSport inatengeneza fedha nyingi na unajua kwa dunia
ya sasa kuwa mapato ya runinga ni sehemu ya tegemeo kubwa la maendeleo katika
klabu.
Angalau kungekuwa hakuna
mkataba kati ya Cecafa na runinga hiyo, tungesema bado haijafikia kuingiza
suala la fedha. Cecafa lazima ibadilike.
Kingine ambacho nimetaka
kukilenga leo ni kuhusiana na suala la nidhamu. Inaonekana Cecafa inajali zaidi
nini kinaingia katika michuano, nasisitiza imekuwa kama mradi wa watu wachache
na haiendeshwi kama baraza makini lenye hadhi ya Ukanda wa Afrika Mashariki na
Kati ambao ndiyo dhaifu zaidi unapozungumzia soka katika bara hili.
Umeona Gor Mahia wamefanya utovu
wa nidhamu mara mbili. Moja wakipita katika geti lisilo sahihi, pili wakavunja
kufuli wakati wakiingia uwanjani.
Cecafa imekaa, baada ya hapo
imeamua kupitisha uamuzi wa kutoa onyo huku ikisisitiza kocha wa Gor Mahia, Frank
Nuttal, anapaswa kuwa makini kwa kuwa naye alikiuka na kuonyesha utovu wa
nidhamu.
Lakini kama ingekuwa
imefanya timu ya Tanzania kama ambavyo tumeona huko nyuma, Cecafa imekuwa
ikikimbilia kutoa adhabu ya faini ya fedha. Vipi kwa Gor Mahia? Hii inazua
maswali kama haya.
Labda kwa kuwa Musonye anatokea
Kenya? Au kwa kuwa Gor Mahia walikuwa hawana hata nauli, hivyo wakipigwa faini
watashindwa kulipa? Au inawezekana kwa kuwa Cecafa ina mpango michuano hiyo ifanyike
Kenya mwakani, hivyo si vizuri kuwaudhi Gor Mahia!
Lazima kuwe na ufuataji wa
kanuni, uhakika na utaratibu bora wa mambo. Kama itaendelea hivi, watu
wakichoka mwisho zitazaliwa Cecafa rundo, moja ya Tanzania, nyingine Rwanda na
Kenya wawe na yao halafu aiongoze Musonye!
0 COMMENTS:
Post a Comment