Kesho Jumapili, Yanga itacheza mechi ya
kirafiki dhidi ya Kimondo FC ya Mbeya, timu hiyo imepania kuonyesha soka safi
kuthibitisha ubora mbele ya winga wao wa zamani, Geoffrey Mwashiuya aliyejiunga
na Wanajangwani.
Yanga inatarajiwa kuondoka jijini Dar es
Salaam, leo Jumamosi tayari kwa mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM
Vwawa, Mbozi jijini Mbeya ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake kwa msimu ujao wa
Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo ni sehemu ya makubaliano ya
kimkataba ya uhamisho wa Mwashiuya aliyejiunga Yanga na kugeuka lulu kutokana na
uwezo wake kuwavutia wengi.
Ofisa Habari wa Kimondo, Chriss Kashililika amesema
timu yao ina jeuri ya kuifunga Yanga kwa kuwa ina kikosi imara kwani ina
wachezaji wanaofanana kiuchezaji na Mwashiuya zaidi ya nane.
“Maandalizi ya mchezo yapo vizuri kwa sababu
timu ipo kambini, Yanga ni timu kubwa na tunaiheshimu lakini kwa jinsi
tulivyojipanga kwa mchezo huo uhakika na ushindi ni mkubwa.
“Kama Yanga walidhani wametukomoa kwa Mwashiuya
basi wanajidanganya, tuna kina Mwashiuya kama nane, kwa hiyo pengo lake
limezibika na tutafanya vizuri,” alijigamba Kashililika na kusisitiza ili
shabiki auone mchezo huo atapaswa kulipa kiingilio cha Sh 5,000.
0 COMMENTS:
Post a Comment