Kocha wa Yanga Mholanzi, Hans Pluijm ameonekana
kuanza kuisuka upya safu yake ya ushambuliaji ya timu hiyo huku akigawa
majukumu kwa mawinga na mabeki wake wa pembeni.
Hiyo ni siku chache tangu timu hiyo iondolewe
kwenye michuano ya Kagame katika hatua ya robo fainali dhidi ya Azam FC kwa
kufungwa kwa penalti 5-3.
Safu hiyo ya ushambuliaji inaongozwa na
Mzimbabwe, Donald Ngoma, Amissi Tambwe (Burundi) na Malimi Busungu huku mawinga
wakiwa ni Simon Msuva, Deus Kaseke, Andrey Coutinho (Brazil) na Geoffrey
Mwashiuya na mabeki ni Hajji Mwinyi na Oscar Joshua.
Kocha huyo, alionekana akiisuka upya kombinesheni
hiyo kwenye mazoezi ya jana Ijumaa, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume
jijini Dar es Salaam akisaidiana na Charles Mkwasa.
Katika mazoezi hayo, Pluijm aliwagawa
washambuliaji hao wawiliwawili na kukimbia golini kwa kupishana kuwahi na kuiunganisha
mipira ya krosi iliyokuwa inapigwa na mawinga.
Ngoma na Tambwe walipangwa pamoja ambao
walikuwa wakikimbia kwa kupishana kuwahi mipira hiyo ya krosi ndani na nje ya
18 kwa ajili ya kuwahi mipira hiyo ya krosi kwa ajili ya kufunga.
Akizungumza baada ya
kumalizika kwa mazoezi hayo, Pluijm alisema kuwa “Katika Kombe la Kagame
nimeona kuna vitu havipo sawa katika safu ya ushambuliaji, ndiyo kama ulivyoona
najaribu kuweka mambo sawa.”
“Nimepanga kuboresha kikosi changu kwa kila sehemu
kwa kuanzia safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji, ninataka timu ifanye
mashambulizi ya kushtukiza kwenye goli la timu pinzani huku tukilinda goli
letu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment