August 10, 2015



Na Saleh Ally
Kampuni ya uchumbaji madini ya Acacia imeidhamini timu ya soka ya Stand United ya Shinyanga kwa udhamini mkubwa unaofikia Sh bilioni 2.

Udhamini ambao wanaupata Stand United kutoka kwa kampuni hiyo ni mkubwa kuliko mwingine wowote wa Ligi Kuu Bara, jambo ambalo ni la kujivunia.

Wanaweza Stand United kuwa wa kwanza kujivunia, lakini ukweli wapenda michezo hasa soka wana kila sababu ya kujivunia kuaminiwa.

Acacia wangeweza kuwa na mambo mengi ambayo wangedhamini nab ado wangeonekana wameisaidia jamii, mfano kununua madawati, vitanda na dawa hospitalini na mambo mengine.

Lakini wakaona soka ndiyo sehemu sahihi ya kupeleka udhamini wao, maana yake ni sehemu wanayoiamini na wanajua watafikia malengo ya wanachokitaka.

Hongera kwa Stand United kuaminiwa, lakini hongera sana kwa Acacia kuamua kudhamini mchezo wa soka kwa kuwa nimekuwa nikipambana kuomba wadhamini wajitokeze.
Uamuzi wa Acacia kuingia katika soka ni sehemu ya mafanikio ambayo wamepata Stand lakini ni mafanikio makubwa kwa wapenda soka kwa ujumla.
STAND UNITED 2014-15

Stand sasa wana deni kubwa kuonyesha timu inapopata udhamini mkubwa inakuwa na nafasi ya kuibua ushindani kama ambavyo tumeona huko nyuma na hadi mambo yanakwenda mbio sasa kwa Azam FC.

Azam FC ni timu ya bilionea namba moja Tanzania, Salm Said Bakhresa ambaye ameonyesha mifano mingi katika uwekezaji na leo inafanya vema. Umeona juzi wamekuwa mabingwa wa Kombe la Kagame.

Stand United hata kama wataenda taratibu, lakini msimu mpya ambao utakuwa wa pili kwao katika Ligi Kuu Bara wanapaswa kuonyesha kwamba udhamini umewasaidia.

Wanapaswa kufanya usajili wa uhakika, benchi la ufundi la uhakika linalofanya kazi zake kwa uhakika pia kambi ya uhakika.

Lakini matokeo pia yawe bora uwanjani baada ya soka la uhakika. Hiyo itachangia hata kuwavutia wadhamini wengine ambao wamekuwa wana hofu kuingia katika soka kutoa fedha zao.
MASHABIKI WA STAND.

Nasisitiza fedha za udhamini ziwe msaada kwa kuwa tuna mifano kadhaa tumeona, wakati timu hazina fedha zimekuwa zikipambana katika ukata zimekuwa zinafanya vizuri.

Lakini inapofikia timu ikapata mafanikio  na pato la kifedha kuongezeka, hapo ndipo matatizo yamekuwa yakianza na hata kusababisha mfarakano mkubwa.

Stand United wanapaswa kuwa makini na kutoingia huko, wafanye vema na kuzisaidia timu nyingine kupata wadhamini zaidi wakati Acacia wakiwa wanajivunia uamuzi wao wa kuingia na kuidhamini timu hiyo ya mkoa wa Shinyanga.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic