Mwomba rufani, Dr. Devota John Marwa, (Mrufani) ni msomi mbobezi katika
taaluma ya michezo, akiwa ni mhadhiri katika kitengo kinachojihusisha na
taaluma ya michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akiamini kwamba anakidhi
vigezo vilivyowekwa kwa nafasi ya mgombea uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
wa Wanawake(TWFA), alichukua fomu ya kuomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa
Chama hicho.
Maombi hayo yalikumbana na pingamizi zilizoletwa na wakereketwa wawili
wa soka la Wanawake, Bi. Chichi Mwidege na Bi. Mwajuma Noty, ambao kwa pamoja
walimwekea pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi matakwa ya kanuni za ugombea wa
nafasi ya Mwenyekiti.
Waleta mapingamizi walidai kuwa Mrufani hakuwa na sifa zilizoainishwa
katika Kanuni za Uchaguzi za T.F.F. (TFF Electoral Code) Ibara ya 9 (tisa)
kipengele cha 3 (tatu), kinachomtaka mgombea awe amejihusisha na uongozi wa
mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
Aidha Ibara ya 28 (ishirini na nane) kipengele cha 3 (tatu), kinamtaka
mgombea awe amejihusisha japo miaka 2 (miwili) katika shughuli za maendeleo ya
mpira wa miguu nchini. Kamati ya Uchaguzi iliridhia mapingamizi hayo na
kuliondoa jina la Mrufani katika orodha ya wagombea wa nafasi hiyo ya
Mwenyekiti. Rufani hii ni matokeo ya uamuzi huo wa Kamati ya Uchaguzi
uliotolewa taraehe 22 Julai, 2015.
Kwa ujumla, sababu za kupinga maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi zinaweza
kuhesabiwa kuwa ni mbili. Moja ni iliyojikita juu ya hitilafu katika kuamua
kwamba Mrufani hakuwa na uzoefu katika uongozi wa soka kwa muda ulioainishwa.
Sabau nyingine ni kwamba Kamati ya Uchaguzi illibua sababu ambayo haikuwa
katika Hati ya pingamizi iliyoletwa na Mleta pingamizi.
Wakati ambapo Mleta pingamizi alijikita katika kipengele cha
28(3), Kamati iliibua kipengele cha 28(8), cha Katiba ya TWFA kinachomtaka
mgombea awe ametimiza uzoefu wa uongozi wa miaka mitano, ambacho hakikuwemo
katika hoja za pingamizi zilizowasilishwa na mleta pingamizi.
Katika kufikia uamuzi wake, Kamati ya Rufani ilizipitia sababu za
Mrufani kama zilivyoletwa, na baada ya kusikiliza maelezo ya Mrufani na hoja za
Mwakilishi wa TFF, Wakili Msomi Edward Augustino, na imeamua kama ifuatavyo.
Tutaanza na hoja ya mwisho.
Je, Kamati ilikuwa sahihi kuibua kipengele ambacho hakikuletwa katika
hati ya mapingamizi? Kamati inaweza kuibua kipengele hicho endapo kwa kufanya
hivyo, itakuwa imejielekeza katika nia njema ya maslahi ya suala
linalozungumziwa.
Sharti jingine ni kwamba hoja hiyo inyoibuliwa isiwe na athari
hasi(prejudicial) kwa mhusika. Kaika suala hili hata hivyo, hoja iliyoletwa na
Mleta pingamizi, yaani hoja chini ya kifungu cha 28 (3), imeainisha kipindi
kifupi cha uzoefu
(miaka 2), na hoja iliyoibuliwa na Kamati inahitaji uzoefu wa miaka 5.
Endapo Mrufani angekuwa na uzoefu wa miaka 3 hadi 4, bado angekwama
kutokana na hoja iliyoibuliwa na Kamati. Hii kwa vyovyote ingekuwa ni athari
hasi (negative impact) katika harakati za Mrufani. Ni vema
Kamati zinazosikiliza malalamiko zikajikita kwenye malalamiko
yaliyoletwa na wahusika wenyewe. Kama pigamizi lingekuwa liko juu ya kipengele
hicho tu, tusingesita kukubaliana na sehemu hii ya rufani. Hata hivyo, takwa la
uzoefu wa miaka 5 limeainishwa pia katika Ibara ya 9 (3), ambayo ilikuwa ni
sehemu ya mapingamizi yaliyokuwepo kwenye hati ya mapingamizi.
Kwa sababu hiyo, Kamati ya Rufani haioni kama hoja hiyo ina mashiko.
Haitaitilia maanani. Hoja kuu ndani ya rufaa hii ni je, Kamati ya Uchaguzi
ilijielekeza vema kuhusu suala la uzoefu wa uongozi ulioainishwa na Katiba?
Mrufani ameieleza Kamati ya Rufani mlolongo wa shughuli ambazo amekuwa
akizifanya, nyingi zikiwa zimejikita zaidi katika taaluma. Miongoni mwa
shughuli hizo ni kuandaa Mpango Mkakati wa kuendeleza soka la wanawake. Mpango
huu uliridhiwa na kuwasilishwa Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira Duniani,
yaani FIFA.
Maelezo mengine ni kushiriki katika kuongoza timu mbali mbali kule Chuo
Kikuu, zingine zikiwa za watoto wadogo ambao baadhi ya matunda yake ni
wachezaji walioibukia kwake kama vile Simon Msuva. Alisema zaidi kuwa
alishiriki kuandaa warsha ilizoandaliwa kwa ushirikiano kati ya FIFA na TFF.
Aidha. Alisema kuwa amekuwa kiongozi tangu akiwa bado kwenye vyuo vya
ualimu, na baadaye alipohitimu na kufanya kazi kama Mwalimu, kabla ya kujiunga
na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliko mpaka sasa. Akasema, hata alipokuwa
Sweden kwa masomo ya juu pia lijihusisha na programu za maendeleo ya soka la
wanawake.
Wakili msomi wa TFF akijibu hoja hizo, alikubaliana na uamuzi wa Kamati
ya Uchaguzi kuwa Mrufani hajaonesha popote kwamba amewahi kuongoza soka,
akasema Mrufani ni mtaalamu tu kama msomi, jambo linaloweza kufanywa na msomi
yoyote. Akamalizia kwa kuiomba Kamati ya Rufani za Uchaguzi kuitupilia mbali
rufaa ya Mrufani kwa kukosa mashiko.
Tofauti na Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani imeona kuwa kwa maslahi
mapana ya mchezo wa soka katika ujumla wake, ni vema kuweka tafsiri pana (wide
interpretation) juu ya sifa zinazozungumzwa, badala ya kuweka tafsiri finyu
(restricted/narrow interpretation) kama ilivyofanya Kamati ya Uchaguzi.
Baada ya kufanya hivyo, kuhusiana na Mrufani, Kamati imeona kuwa ana
sifa zinazostahili. Kupitia sababu alizozitoa, na vielelezo vyake, Kamati ya
Rufani haina wasiwasi kuwa Mrufani ana uzoefu mbali mbali sio katika soka tu,
bali pamoja na michezo katika ujumla wake.
Tumeshuhudia katika maelezo yake kwetu kwamba ushiriki wake katika hatua
mbali mbali, japo hakuwahi kuchaguliwa, sio ushiriki wa kitaaluma tu, kama
msomi mwingine yeyote. Ni ushiriki wenye dhamira ya dhati ya kuleta
mabadiliko/maendeleo katika soka la wanawake. Maelezo
yake kuwa aliaandaa programu ya maendeleo ya soka la wanawake,
hayakupingwa. Kamati ya Uchaguzi ingeangalia namna ambavyo “visheni” iliyomo
katika programu ile ambavyo ingeweza kutekelezwa na mtu aliyeaiandaa. Kwa hiyo,
katika hoja hii, Kamati inakubaliana kuwa Mrufani
anazo sifa stahiki, na kukatwa kwa sababu hii, Kamati ya Uchaguzi
haikujielekeza vema. Kwa hiyo, Mrufani ameshinda rufaa yake? Kamati ya Rufani
inachelea kujibu swali hili moja kwa moja. Utaratibu wa kuwasilisha rufani
ulikiukwa, na hapa ndipo rufaa hii inapokwaa kisiki. Chini ya Ibara ya 13
(1) cha Kanuni ya
Uchaguzi (Electoral Code), mgombea ambaye hakuridhika na maamuzi,
atawasilisha rufaa yake ndani ya siku 3 (tatu) tangu uamuzi anaoupinga
ulipotolewa.
Kipengele cha 3 (tatu) cha ibara hiyo kinasema kwamba Mrufani yoyote
atakuwa na uhalali endapo rufaa yake imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni
hizo. Uamuzi unaolalamikiwa ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu za
rufaa ziliandaliwa tarehe 27 Julai na sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe 28
Julai, 2015. Ni dhahiri kwamba rufaa ililetwa nje ya muda uliowekwa na kanuni,
na kwa hiyo inakosa uhalali kisheria na kikanuni.
Japo katika mwenedo na maamuzi yake Kamati ya Rufani za Uchaguzi
haifungwi na taratibu za kimahakama, suala la muda wa kuwasilisha rufani sio
miongoni mwa mambo ambayo Kamati inaweza kutoyazingatia. Kwa sababu hiyo, Rufaa
hii imetupwa, lakini kwa sababu tofauti na zile za Kamati ya Uchaguzi.
Pamoja na uamuzi huu, Kamati ya Rufani za Uchaguzi inapenda kwa namna ya
kipekee kumpongeza Mrufani kwa jitihada alizozionesha kutaka kuitumikia TWFA.
Ni matumaini ya Kamati kuwa hatokata tama, na kwamba atakuwa tayari, akitakiwa
kufanya hivyo, kupitia taalum yake, kushirikiana na wenzake katika jitihada za
kuendeleza soka la akina mama lililo na changamoto lukuki.
Imetolewa na,
JULIUS M. LUGAZIYA
Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za Uchaguzi
0 COMMENTS:
Post a Comment