MGOPE... |
Wadau, tunapenda kusahihisha baadhi ya taarifa zinazosambaa
kuhusiana na urushaji wa mechi za VPL (Vodacom Premier League) na La Liga.
Katika mkutano wetu na bodi ya Ligi kuu Tanzania (TPLB)
tarehe 15 Septemba 2015, AzamTV iliiomba bodi kufikiria kubadili muda wa kuanza
mechi za ligi katika siku za Jumamosi na Jumapili ili kuruhusu urushaji wa
mechi nyingi zaidi za moja kwa moja (live).
Hivi ndivyo jinsi ligi za nchi za barani Ulaya
zinavyofanya ili kuhakikisha wapenzi wa soka wanashuhudia mechi kadhaa ndani ya
siku moja. Kwa mfano, mechi tatu za EPL huruka muda tofauti katika siku moja.
Kama hapa nyumbani Tanzania, mechi za ligi nazo
zingepangwa kuanza muda tofauti kama wanavyofanya wenzetu, kwa mfano mechi zingeanza
saa 8:00 mchana, Saa 10:00 alasiri na saa 12:00 jioni, basi wapenzi wa soka
wasingepata shida kuchagua mechi gani ya kuangalia na badala yake kuangalia
mechi zote 3. Kuliko ambavyo watakapokuwa na wakati mgumu wikiendi hii ambapo
mechi zote zitaanza saa 10:00 alasiri.
Hii ina maanisha, si wapenzi wa soka tu watakaofaidika
na mabadiliko haya, bali fursa hii ya kuonekana moja kwa moja (live) kwenye TV
itaongezeka maradufu kwa wachezaji, klabu zao, pamoja na wadhamini wao. Vile
vile hii inamaanisha kwamba sio timu kubwa tu zitakazofaidika, bali timu zote
kwenye ligi ya VPL zitapata nafasi ya kuonyesha ujuzi wao mbele ya wadau na
wapenzi wa soka.
Hizi mechi zitaonyeshwa kupitia chaneli ya Azam One na
Azam Two ambazo mbali ya kupatikana ndani ya Tanzania, pia huonekana katika
ukanda wote wa Kusini wa jangwa la Sahara katika nchi ambazo AzamTV
inapatikana. Kwa hiyo kuongeza fursa ya kuonekana ndani na nje ya Tanzania. Tumefurahishwa
na bodi ya Ligi kuu Tanzania kuonyesha ushirikiano katika kuunga mkono hoja hii
na wataendelea kulifanyia kazi pamoja nasi ili kufanikisha ratiba ya aina hii.
Wateja wetu wa chaneli ya Azam Sports HD (ambayo
inapatikana Tanzania tu) nao watapata fursa ya kuangalia baadhi ya mechi hizi
katika ubora wa HD.
Chaneli ya Azam Sports HD ni chaneli maalum inayoonyesha
mechi za ligi ya Hispania (La Liga) ndani ya AzamTV. Hata hivyo taarifa za
kizushi zilizoenezwa kwamba, tumependekeza ratiba hii ili kuitangaza zaidi La
Liga kuliko VPL, hazina ukweli wowote.
Mechi zote za Ligi kuu ya VPL zitarushwa kupitia chaneli
zetu mbili za kimataifa – Azam One na Azam Two. Hii inamaanisha wateja wetu
wote watapata nafasi ya muendelezo wa mechi kuanzia saa nane mchana mpaka saa
sita za usiku kila mwisho wa wiki kwa kipindi chote cha msimu wa Tanzania,
Afrika Mashariki na Hispania.
MGOPE KIWANGA
MKUU WA MASOKO NA MAUZO
AZAM MEDIA GROUP
0 COMMENTS:
Post a Comment