MECHI ya watani ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu
kubwa na mashabiki wa soka nchini. Sasa ni uhakika, kwamba Yanga wameshinda kwa
mabao 2-0 na wanaendelea kusherekea.
Simba
waliokuwa wababe wa Yanga, wamepoteza ile sifa yao kwamba wakikutana na watani
wao, kwa ulaini wenyewe ‘wanajipigia’ tu. Sasa hakuna tena, inabidi wasubiri
hadi watakapokutana mzunguko wa pili.
Mechi ilikuwa nzuri, hakika Simba
walionyesha soka safi hasa katika kipindi cha kwanza lakini wakashindwa
kuzitumia nafasi nzuri katika kipindi cha kwanza ambazo zingeweza kuwapa
matokeo tofauti.
Lakini Yanga wakaonyesha kweli wana wachezaji
wengi wazoefu ambao waliweza kuihimili presha hiyo ya Simba hadi walipofanikiwa
kufunga na baadaye kuyabadili kabisa mambo hadi walipoibuka na ushindi.
Kitu kizuri ni kwamba asilimia 99, watu
wameondoka hata bila kuingia kwenye tafrani na ninaamini walifika nyumbani
salama ambalo ni jambo jema.
Kikubwa ninacholenga leo, si kigeni na mara
kadhaa nimekuwa nikizungumzia au kukikemea, mchezo wa kihuni, tena uhuni wa
kijinga.
Nianze na kukumbushia mambo kadhaa ambayo
hata nilipoyazungumzia nilionekana ninaitetea timu fulani ingawa sioni haja ya
kujitetea katika hilo.
Kipindi kile yule beki wa Ruvu Shooting, George
Michael alipomkaba Amissi Tambwe wa Yanga. Lakini unakumbuka beki Juuko Murshid
wa Simba alipompiga kiwiko mchezaji wa Mgambo kama sijakosea.
Kumekuwa na matukio mengi ya namna hiyo
ambayo si ya kiungwana na yanaendelea kujitokeza kwa kasi kwenye mchezo wa soka
nchini.
Juzi, mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma,
licha ya kuwa ni mrefu mara moja na nusu kwa beki Hassan Kessy wa Simba,
aliinama na kumpiga kichwa wakiwa hata hawagombei mpira.
Katika hali ya kawaida kabisa, mwamuzi
mmoja, hasa kati ya hawa wawili, mmoja wao atakuwa aliona, yule wa kati au
msaidizi wa kwanza.
Lakini ajabu, hakuna hatua iliyochukuliwa na
kunakuwa hakuna ushahidi wa kumkamata mwamuzi huyo na kumlazimisha kuwa aliona.
Anaweza kufanya hivyo yaani kujikausha ili kuepusha lawama kwamba aliharibu
mchezo.
Mwamuzi Israel Nkongo inawezekana aliona
lakini mawazo kwamba mchezo ni mapema mno, au watu hawawezi kuamini kama kweli
Ngoma alifanya vile basi ikachangia yeye kujikausha, jambo ambalo ni baya
kabisa kama kweli atakuwa aliona.
Lakini kuwasaidia Nkongo na wenzake kwa kuwa
ni binadamu, TFF sasa inalazimika kurekebisha kanuni zake ziwe na makali zaidi
kwa wachezaji wenye uchezaji wa kihuni, wa kijinga, usio wa kiungwana na wa
kibabaishaji kama alioufanya Ngoma.
Mimi pia ninaweza kuwa kama Nkongo kama
kweli hakuona tukio hilo. Kwamba huenda kuna matukio mengine ya kijinga na
yasiyo ya kiungwana yalijitokeza.
Si sahihi hata kidogo, mchezaji kumpiga
mwenzake pigo lisilo la kimichezo, tena wakiwa bila mpira. Hivi hawa wachezaji
wa kigeni nao ndiyo wanachokileta hapa?
Ngoma ni mchezaji mwenye uwezo mzuri, lakini
kama ataendelea hivyo, atafeli na mwisho ataacha wengine aliowakuta wakitamba.
TFF lazima ikubali kwamba huu ndiyo wakati kanuni zinaweza kubadilika na
wakaanza kutumia picha za video kufanya uamuzi na kutoa adhabu kwa watu wenye
tabia chafu zisizokuwa za kimichezo.
TFF inaweza kuwa na uhakika wa matumizi wa
kanuni hiyo kwa kuwa sasa kuna Azam TV ambayo inaonyesha mechi za Ligi Kuu Bara
tena kwa ufanisi mkubwa huenda hata kuliko ilivyokuwa zikionyesha runinga
nyingine zikiwemo za nje.
Azam TV ni wadhamini wa Ligi Kuu Bara. TFF
wanaweza kuzungumza nao na kuchukua karibu kila mechi inayoonyeshwa na
kuifanyia kazi kama kuna malalamiko au la.
Najua walitumia picha za Championi kumpa
adhabu beki Michael kutokana na mchezo wake usio wa kiungwana dhidi ya Tambwe
msimu uliopita.
Bado kuna haja ya kuongeza ukali wa adhabu
kwa kubadili kanuni ili ikiwezekana kuondoa kabisa uhuni ‘vumbi’ unaofanywa
katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Acha ushabiki mdogo wangu Saleh,unakuwa kama yule kubwa ji-nga mtoto wa mchezaji maarufu wa zamani!?Wakati Kessy anamkwatua Ngoma na kuanguka kama zigo na pia Is-haka kumkanyaga mkononi na kutokea purukushani uwanjani,wewe uliona sawa.Kwani kumkanyaga mwenzio mkononi akiwa amelala chini ni kitendo cha kiungwana?Mbona wewe hukemei hilo?
ReplyDeleteKuna wakati nyie washika kalamu mnazidiwa na mahaba na kushindwa kuendana na taaluma yenu ndio maana watu wanawanunua kwa bei rahisi sana!
Hao wote wanastaili adhabu kali ili iwe fundisho si kwa adui yako nyoso tuu na hao akina Kessy.Mpira ni taktiki lakini si kuwatumia washika kalamu kama wafanyao Lunyasi!
Kaka salaam . Ni kweli kuwa ngoma alimpiga kichwa mchezaji wa sharubu na ni kosa ila maelezo yako kama una chuki ndani ya moyo wako . Sijaona sababu ya ww kusema mchezaji toka nje anafanya ubabaishaji unaweza kuniambia ni ligi gani duniani isiokua na mikimiki kama hiyo ya kupigana wacha ushabiki na kusema kisa mgeni hata akiumizwa akae kimya . Wageni wangapi ulaya wanapigana viwanjani umesahau cantona di canio hata wachezaji bora duniani hupigana kina zidane sembuse ngoma wacha ushabiki usio na tija. Kaka mm ni mpenzi wa blog yako ila huu upenzi hauna maana ... soka ni mchezo wa vita hasa damu inapokua ishachemka . Wacha kutaka kutupumbaza eti uhuni usafishwe asilimia 70 wacheza soka ni watoto wa mitaani walolelewa kwenye ugumu unadhani watakosa ubabe. Yapo matukio ya kulalamikia kama kushikana makalio ila sio kichwa ni kawaida kwenye soka. Msitumie kalamu na karatasi na blog zenu kutaka kutupumbaza wote tunaangalia soka na tunajua yanayotokea msijifanye wachambuzi hata danadana kumi hupigi. Asante na nitaendelea kusoma blog yako.. Yanga mbele mbele daima nyuma mwiko
ReplyDeleteWachezaji wa kigeni wanafanyiwa uhuni sana ili washindwe kucheza mpira!! Simba walimchukulia Ngoma kama mchezaji hatari na walitumia nguvu nyingi kumdhibiti ikiwemo kumtisha na kumfanyia rafu mbalimbali tena nyingine akiwa hana mpira. Nakumbu Nonda Shabani aliwahi kuhojiwa na BBC na akakiri kuwa wachezaji wa kitanzania hawafanikiwi kwa kuwa wana tabia ya kuwachezea kihuni wachezaji wa kigeni!! Na akatoa mfano wa mechi moja morogoro alishikiwa msumari na beki wa timu pinzani kitu kilichomfanya akashindwa kucheza mpira!! Tusitumie taaluma zetu kueleza mapenzi na ushabiki badala ya kuzungumzia uhalisia ili kuinua wachezaji wetu
ReplyDeleteWewe mwenyewe unaonyeshaa ubaguzi wa wazi kwa wageni.
ReplyDelete