Kazi ipo! Yanga imesema itaitafuta haki yake kwa mshambuliaji Geilson Santana 'Jaja' hadi nchini kwao Brazil.
Yanga imefungua kesi mahakamani kudai dola 300,000 ikidai Jaja ambaye alijiunga nayo msimu uliopita kwamba alikiuka mkataba. Kwa sasa raia huyo wa Brazil yuko nchini kwao akiendelea na maisha yake.
Mwanasheria wa Yanga, Frank Chacha amesema kuna mahakama nchini Brazil inaweza kuwasaidia kukazia hukumu ya Jaja ili haki yao Yanga ipatikane.
Chache amesema hayo leo baada ya kesi Yanga dhidi ya Jaja kuahirishwa kutokana na tatizo la kuzimika kwa umeme nchini.
"Kesi imeahirishwa kutokana na tatizo la umeme, lakini bado Jaja hakutokea mahakamani na licha ya kumfikishia taarifa bado amekuwa akipiga danadana.
"Bado tuna uhakika wa kupata haki yetu hadi Brazil, kuna mahakama ambayo inaweza kukazia hukumu nchini humo kulingana na mambo yatakavyokwenda katika kesi ya hapa.
"Lengo ni kupatikana kwa haki ya Yanga, jambo ambalo tunaamini litafanikiwa," alisema Chacha.
0 COMMENTS:
Post a Comment