Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo
limeingia mkataba wa miaka mitatu wenye thamani ya shilingi milioni mia nne
hamsini (450,000,000), na kituo cha luninga cha Star Tv kurusha matangazo ya
Ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL).
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kusaini
mkataba huo, Rais wa TFF Jamal Malinzi aliishukuru kampuni ya Sahara Media
Group kwa kuamua kuwekeza katika mpira wa miguu nchini kwa kuamua kuonyesha
ligi daraja la kwanza.
Malinzi ameviomba vilabu vya FDL kutumia udhamini huo
kama chachu ya mafanikio na kufanya vizuri katika ligi hiyo itakayotoa timu
tatu za kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (FDL) msimu ujao.
Aidha Malinzi amewaomba wamiliki wa viwanja
vinavyotumika kwa michezo ya FDL kuviweka katika hali nzuri ya matunzo ili
mechi zinazochezwa katika viwanja hivyo ziweze kuwa nzuri kiufundi na muonekano
wa kwenye Luninga.
Jumla ya udhamini wa Ligi Daraja la Kwanza kwa sasa ni
shilingi bilioni moja na milioni mia tatu hamsini (1,350,000,000) ikiwa ni
udhamini wa milioni mia tisa (900,000,000) kutoka StarTimes mdhamini mkuu
wa FDL na milioni mia nne hamsini (450,000,000) kutoka StarTv.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Sahara Media Group, Samwel
Nyala ameishukuru TFF kwa kuwapa nafasi hiyo ya haki za matangazo kampuni yake
kwa michezo ya Ligi Daraja la kwanza nchini (FDL).
Katika kuhakikisha michezo hiyo inaonekana kwa wingi
zaidi, Nyala alisema watafungua mkondo (Channel) ya Star Sports Plus itakayokua
itakayokuwa inaonyesha michezo tu ikiwemo ligi daraja la kwanza (FDL).
Akiongea kwa niaba ya vilabu ya ligi daraja la kwnza
nchini (FDL), Asha Kigundula - Afisa habari wa klabu ya Friends Rangers ya
jijini Dar es salaam, ameishukuru TFF kwa kuweza kuwapatia udhamini kwenye
ligi, jambo ambalo litawapelekea kujiandaa na kufanya vizuri katika ligi msimu
huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment