November 23, 2015


Na Saleh Ally
DIRISHA la usajili limefunguliwa kutokea Novemba 15 hadi Desemba 15 na kila timu inayotaka kufanya usajili inatakiwa kuwa imekamilisha kila kinachotakiwa.


 Usajili ni sehemu mpya kwa timu kujirekebisha na kufanya kile ambacho inaona kimepungua katika kikosi chake kwa ajili ya kumalizia ligi.

Kwangu nimekuwa ninaona kama kuna kitu ambacho hakipo sawa. Kwamba dirisha dogo la usajili linafunguliwa mapema sana.

 Kweli karibu kila timu inakuwa imeona upungufu ambao inaweza kuufanyia kazi. Lakini angalau kungekuwa na idadi ya kutosha ya timu huenda kungeweza kuwa na mabadiliko bila ya kuingia gharama.

 Wakongwe Simba na Yanga, katika misimu miwili wameingia kwenye rekodi ya timu ambazo zimefanya usajili wake kwa kukurupuka, tena kwa kiasi kikubwa na mara nyingi wamekuwa ni wagumu kukubali.

Yanga wanaweza kuwa na angalau, Simba wakawa walivurunda zaidi lakini hakuna anayeweza kukwepa kwamba kuna mambo mengi sana hayakuwa sawa katika suala la usajili.

Beki Vincent Bossou, raia wa Togo, amejiunga na Yanga lakini alijikuta akikaa benchi zaidi ya mechi tano akiangalia Watanzania wakiendelea kucheza, jambo ambalo halikuwa sawa hata kidogo.

Hali kadhalika Simba tuliona, mshambuliaji Pape N’daw kutoka Senegal, naye alilazimika kusubiri katika benchi la Simba na hata siku alipopewa nafasi ya kuingia, ikawa ni sawa na uigizaji wa kipindi cha komedi.

 Maana aliingia na viatu vikuukuu na mwisho akasema ni bahati, siku chache baadaye akakamatwa akiwa na hirizi ambayo tuliibandika jina la Power Bank. Hakuna alichoifanyia Simba ambayo imeishia kumlipa dola 3,000 (zaidi ya Sh milioni 6) ili aondoke.

 Utakumbuka msimu mmoja kabla, Simba iliwasajili wachezaji wa kigeni na kuwaacha ndani ya msimu mmoja. Sasa imewaacha wachezaji hata kabla ya nusu msimu kufika. Hili si jambo zuri kwa wanaohusika na usajili na lazima wakubali kutuacha tuseme kwa kuwa vitu walivyofanya si sahihi.

 Inawezekana ni kosa la kocha, kosa la mjumbe wa kamati ya usajili au vinginevyo. Lakini ukweli ni kwamba, kosa limefanywa na Simba na kamwe hawawezi kulikimbia.

Makosa yamekuwa mengi, hakuna sababu ya kusajili mchezaji wa kigeni anayelipwa kwa dola halafu anaendelea kukaa benchi, si sahihi.

Mbrazili, Coutinho wa Yanga, bado hana faida kubwa kwa kuwa kocha anaonekana hamkubali katika programu zake. Anatumia muda mwingi benchi huku akichota mamilioni ya fedha kuliko wale wanaocheza, hakika bado hili si jambo zuri na lazima liangaliwe.
Wachezaji wa kizalendo wengi wanaumia, tatizo lao ni moja. Waoga, hivyo hawawezi au hawako tayari kuanika ukweli kwamba wanaona wanatumika, wanapambana kwa ajili ya klabu na timu kwa ujumla lakini wanaolipwa zaidi wanaonekana hawana msaada kama walionao wao.
Kuna mengi yanawezekana kushindana kuepushwa yasitokee katika kipindi hiki cha usajili hasa kama Simba, Yanga, Azam FC na klabu nyingine zitafanya usajili. Hauwezi kuepusha wachezaji kukaa benchi kwa kuwa wote hawawezi kucheza.

Lakini vigezo vinabaki palepale, wachezaji wa kigeni lazima wawe na ubora ulio juu zaidi, msaada wa juu ni funzo au changamoto kwa wachezaji wengine wazalendo. Lakini si waje hapa nyumbani kuuza sura kwenye benchi huku wakichota mamilioni ya fedha kuliko wazalendo tena wanaoonekana wana msaada mkubwa zaidi katika vikosi vyao.

 Najua kusema maneno ya kukosoa inauma sana, lakini tukubaliane jambo hili. Kama klabu zitaendelea kusajili wachezaji wa kubahatisha, basi hofu ya kwamba kuna “dili” zinapigwa kufaidisha mifuko ya watu, zitakuwa ni sehemu ya hoja.

 Kukosea mara moja au mbili angalau, lakini kuendelea kukosea kila mara mambo yanayofanana si jambo sahihi. Lazima mtasababisha hali ya hofu kuhusiana na ukweli. Acha tuwape nafasi.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic