Na Saleh Ally
SUALA la viwanja limekuwa ni sawa na gumzo la
kawaida kabisa kama unazungumzia mpira wa Tanzania. Hakuna kiongozi anayeona
kwamba ni jambo kubwa sana.
Kumekuwa na mazoea makubwa kwamba timu
zinazoshiriki hata ligi za juu kama Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Kuu Bara nazo
zinaweza kuendelea kufanya mazoezi kwenye viwanja vya ‘kuokoteza’.
Mfano viwanja vya shule za msingi au sekondari
au viwanja vingine ambavyo vinakuwa ni kwa ajili ya watoto au vijana.
Hii imekuwa ni kawaida kabisa na hali hii
inaonekana kuzoeleka karibu kwa kila timu huku ikionekana timu kutokuwa na
uwanja ni jambo la kawaida na si kulishangaa.
Hiki ni kitu ambacho hakionekani kuwa ni
kibaya au cha hovyo kwa kuwa viongozi wengi wa soka wamekuwa wakifanya mambo
kwa kulipua na wenyewe wanaona ni sawa kwa kuwa si wanaowaza kuleta maendeleo.
Kila kiongozi anaamini kulipa kiasi cha fedha
ili timu yake ikafanya mazoezi ni sahihi kuliko kujenga uwanja au kutengeneza
angalau uwanja wa mazoezi tu.
Kichekesho hiki kimeendelea kuvunja
mbavu kila kukicha. Viongozi wanaendelea kutembea kila siku na katika nchi
mbalimbali wanakutana na changamoto za kuona kila klabu ina uwanja angalau hata
wa mazoezi.
Wameona karibu kila nchi, suala la uwanja wa
mazoezi ni lazima. Kuwa na klabu ya soka bila uwanja wa mazoezi kwa ajili ya
timu ni kichekesho na sehemu ya kuonyesha hakuna nafasi kwa Tanzania kupiga
hatua mbele kwa kasi.
Bado viongozi wanaliona na kuliacha,
ndani yake pia utasikia watu wanazungumzia suala la maendeleo ya vijana ambalo
kamwe halitawezekana.
Tumeona Yanga na hata Simba wakilazimika
kupunguza idadi ya mazoezi kutokana na gharama za kulipia viwanja.
Wakati mwingine makocha wamekuwa
wakilazimishwa kufanya mazoezi mara moja kwa siku wakati wangependelea kufanya
mara mbili.
Nakukumbusha Kocha Ernie Brandts aliyekuwa
akiinoa Yanga alivyolalamika kutafutiwa magoli madogo lakini hakuyapata hadi
alivyoondoka. Nakukumbusha alivyolia kuhusiana na ubovu wa viwanja kwamba
anashindwa kufundisha anachokitaka kwa kuwa mpira hauwezi kutembea chini.
Tunalalamika tuna wafungaji wasio na uwezo.
Tunajua pamoja na vipaji lazima kuwe na mafunzo ambayo pia vigumu kupatikana
kwenye hali ya viwanja tulivyonavyo.
Jiulize katika hali ya kawaida, kwa nini tushindwe
kuwa na viwanja? Tunakosa nini hasa hadi kuwa na viwanja liwe ni jambo gumu
sana kiasi cha kuwa gumzo lisilokuwa na utatuzi?
Ardhi tunayo, majani yapo, hata maji
yanapatikana. Hapa ni fedha za utengenezaji na mtu wa uangalizi. Sasa hili
linashindikana kwa timu kama Simba. Tena ajabu zote mbili zina viwanja na kila
kitu, bado majani na mtu wa uangalizi pekee?
Klabu nyingine pia zinapaswa kuliangalia hili.
Ukombozi wa soka nchini bado, lakini suala la viwanja ni lazima lifanyiwe kazi
na hakuna sababu ya kuwa na mzaha au viongozi kusubiri hadithi au kuendelea
kukubaliana na utaratibu huu.
Inawezekana kabisa viongozi wamekubali kufeli
kwa miaka yote lakini inapendeza huu wa 2015 ukawa mwisho na baada ya hapo
mabadiliko yaanze na viwanja.
Klabu zibadilike, viongozi wawe na ndoto
kweli ya kuendeleza soka badala ya maneno. Tukubaliane bila ya viwanja,
maendeleo sahihi ya soka yatakuwa ni hadithi tu.
Viongozi acheni maneno mengi, kweli
nendeni na program ya muda. Halafu angalieni program ya muda mrefu na tukubali
hakuna mafanikio kimataifa kama tutabaki hapo tulipo na klabu zetu mataji ya Ligi
ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika yataendelea kuwa ni hadithi tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment