HAJI MANARA |
AWALI ya yote niwape hongera wana Simba wote
kwa uvumilivu mkubwa mlionao, hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho mnapitia.
Kipindi kigumu kwa maana mbili kubwa. Kwanza
najua wengi hamridhiki na nafasi tuliyopo hivi sasa kwenye msimamo wa ligi kuu
inayoendelea nchini na pia wengi mmekuwa na sintofahamu kuhusu masuala
mbalimbali yanayoendelea nje ya uwanja, hususan suala la kuvamiwa kwa eneo
linalotarajiwa kujengwa uwanja linalomilikiwa na Klabu ya Simba kule Bunju
jijini Dar es Salaam.
Naomba nianze na suala la wapenzi
kutoridhika na maendeleo ya timu uwanjani, hususan kuwa kwenye nafasi ya nne
kwenye msimamo wa ligi kuu.
Siyo siri, Simba inapita katika kipindi
kigumu sana, lakini kiukweli nafasi tuliyopo kimsimamo, siyo mbaya hata kidogo,
ukilinganisha na klabu zilizopo juu yetu.
Tofauti yetu na timu inayoongoza Ligi Kuu
Tanzania Bara ni pointi nne tu huku kila timu ikiwa imecheza michezo tisa.
Wapo wanaosema timu haichezi soka
linaloburudisha, pia wapo wanaokwenda mbali zaid kwa kusema kwenye safu ya
ushambuliaji kuna udhaifu mkubwa.
Kwa jicho langu, kuna eneo nakubaliana na
baadhi ya mitazamo ya wakosoaji, ila niwaambie uongozi unazijua changamoto zote
hizo, hususan kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ambayo hata Kocha wa Simba,
Dylan Kerr alitaka hivyo.
Taarifa njema kwa wana Simba ni kurejea kwa
mchezaji wake Mkenya, Paul Kiongera, aliyekuwa kwa mkopo kwenye timu ya KCB ya
nchini Kenya.
Lakini pia usajili wa Brian Majwega,
mchezaji wa kimataifa wa Uganda aliyekuwa Azam FC, naye ataanza rasmi
kuitumikia Simba mara ligi itakapoanza kwenye raundi ya kumi baadaye mwezi huu.
Mimi naamini kwa usajili huu, Simba itakuwa
imepata suluhisho kwenye safu yake ya ushambuliaji, ukizingatia kupatikana kwa Hati
ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mshambuliaji wetu, Danny Lyanga, sambamba na
usajili wa beki mpya kutoka timu moja inayocheza ligi kuu nchini.
Naamini kwa usajili huo, ukichanganya na majembe
yetu tuliyonayo, tutafanya vizuri msimu huu.
Tunachoahidi ni kuwapa matarajio yenu, tena
kwa nguvu zote, la kuomba ni uhai tu.
La pili, nililopanga kuwaambia kwenye barua
hii fupi, ni suala la uwanja wetu uliopo Bunju.
Zimeibuka porojo nyingi kuhusu uwanja wetu
wa Bunju kuvamiwa na baadhi ya watu ambao wamejenga nyumba kwenye eneo hilo.
Binafsi nilipoziona hizi taarifa kwenye
baadhi ya vyombo vya habari, nilishtuka sana, hata Rais wa Simba, Evans Aveva,
naye alishtuka kupita kiasi na kuamua kuondoka mwenyewe kwenda kujionea
kinachoendelea huko.
Kimsingi hakuna mtu au kikundi chochote ambacho
kimevamia eneo hilo. Kilichoonekana kwa baadhi ya waandishi waliokwenda eneo
hilo ni kuzionyesha nyumba zilizopo pembeni ya eneo la Simba na kusema kuwa
zimejengwa ndani ya eneo letu, lakini siyo kweli.
Wakati mwingine najiuliza unawezaje kujua
mipaka sahihi kama siyo kuwauliza wamiliki halali wa eneo husika au watu wa
manispaa na wale wa ardhi?
Ni kuikosea heshima klabu kwa kiwango cha
juu kuandika habari bila kufanya utafiti na kuwaweka wapenzi wetu roho juu bila
sababu yoyote ya msingi.
Ninalowaomba wanachama na wapenzi wetu, wapuuze
hizo taarifa, ni uongo mkubwa.
Matarajio yetu ni kuona habari za upotoshaji
wa aina hiyo hazijirudii tena na sisi tutaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo
vyote vya habari kwa kuzingatia misingi ya uandishi na utamaduni wa klabu.
Mwisho niishukuru timu ya Gazeti la Championi
kwa kunipa fursa hii adimu ya kuongea na Wanasimba wenzangu kupitia safu hii.
Naamini Mhariri Kiongozi na rafiki yangu Saleh
Ally, utanipa fursa tena na siyo kuongea na Wanasimba tu bali kutoa mchango
wangu kwenye maendeleo ya mchezo huu murua zaidi duniani.
Adioss...
Makala haya kwa mara ya kwanza yalichapishwa jana katika gazeti Bora la Michezo Tanzania la CHAMPIONI.
0 COMMENTS:
Post a Comment