Baba mzazi wa straika wa TP Mazembe, Mbwana Samatta, Ally Samatta, amemuandalia mwanaye sherehe ya kufa mtu mara baada ya kutua nchini akitokea Lagos, Nigeria.
Sherehe hiyo inakuja baada ya Samatta kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza barani Afrika. Samatta alitarajiwa kuwasili usiku wa kuamkia leo Jumamosi.
Mzee Samatta alisema anamshukuru Mungu kwa kumjaalia kijana wake kuchukua tuzo hiyo kwani ni wazi anafuata nyayo zake kutokana na yeye mwenyewe kuwahi kuwa Mchezaji Bora wa Tanganyika mwaka 1964.
“Mara baada ya kumpokea uwanja wa ndege, kama familia tumemuandalia sherehe ya kumpongeza, amefanya jambo kubwa kwa familia na taifa kwa ujumla, anapaswa kupongezwa.
“Katika sherehe hiyo tutakula na kunywa pamoja, ukoo mzima wa Samatta utakuwepo, si unajua kila mmoja ana baraka zake, naamini baada ya hapo safari yake ya kwenda Ulaya itakuwa ya mafanikio zaidi,” alisema mzee Samatta.
0 COMMENTS:
Post a Comment