January 25, 2016


Mechi tatu, ameshinda zote, hajafungwa bao lolote. Huyu ni Jackson Mayanja ambaye alisaini Simba kama kocha msaidizi lakini taarifa zimesema uongozi wa klabu hiyo umeamua awe kocha mkuu hadi mwisho wa msimu.

Mayanja amepewa mikoba hiyo kutokana na mazungumzo kati ya Simba na kocha Mdenishi, Kim Poulsen kukwamia kwenye suala la maslahi na dili la Hemed Morocco nalo kufa dakika za mwisho, baada ya kuahidiwa atalipwa mshahara wa Sh milioni tano, lakini alipotua Dar wakageuka, wakaziona nyingi na wakamuwekea mezani Sh milioni nne, akachomoa, akabeba mabegi yake na kurudi zake Zenji.

Pia taarifa zinasema uongozi wa Simba unaridhishwa na mwenendo wa timu hiyo kwa sasa ikiwa chini ya Mganda huyo ambaye ameonyesha mabadiliko makubwa kiasi cha kumfunika Muingereza, Dylan Kerr.

Mchezo wa kwanza kwa Mayanja ulikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar ambao alishinda bao 1-0, kisha akashinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu kabla ya juzi Jumamosi kushinda mabao 3-0 dhidi ya Burkina Faso kwenye Kombe la FA ugenini.

Mratibu wa Simba, Abass Ally, amesema: “Kikubwa ambacho mpaka sasa unaweza kumzungumzia Mayanja, amefanikiwa kutatua tatizo la fitness na ndiyo maana timu inaonekana kuanza kucheza soka dakika 90, tofauti na ilivyokuwa kwa Kerr. Awali ilikuwa haiwezi kufika dakika 90, lakini angalau kwa sasa unaona timu inapambana na inacheza soka linaeleweka muda wote.”

Kwa upande wa Mganda huyo alisema mfumo wake ni soka la kusaka mabao na siyo kupaka rangi mipira pamoja na kuhakikisha wachezaji wanacheza wakiwa na pumzi ya kutosha muda wote.

“Kwa kipindi hiki, najaribu kuwarudisha wachezaji kwenye utimamu wa kucheza dakika zote. 

Napenda kuona soka la kusaka magoli na timu kupigana mwanzo-mwisho, hiyo ndiyo falsafa yangu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Coastal Union, Kiyovu ya Rwanda na timu ya taifa ya Uganda.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic