January 29, 2016

MALINZI

Na Saleh Ally
NAAMINI huwa unasoma kila ninapozikosoa Yanga na Simba kutokana na mambo kadhaa, leo nataka uendelee kusoma nikizitetea tena bila ya woga, kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni dhaifu, watu wake ni dhaifu na si watendaji bora.

Asilimia 90 ya watendaji wa TFF hasa wale wanaohusika na masuala ya mchezo wa soka, mfano mashindano, timu za taifa, ni watu ambao wako katika nafasi ambazo si saizi yao na hawawezi kuzitendea haki kwa maana ya utendaji bora.

Kusema ukweli ni kuwa adui, kuwa tishio la ajira za ujanja za watu lakini hakika lazima niendelee kupiga gitaa bila ya woga ili siku moja ikiwezekana mbuzi afikie acheze tu.

Kadiri siku zinavyosonga mbele, taratibu nimeanza kuona nakuwa mzoefu na mjuzi zaidi wa upigaji gitaa. Najua ndugu zangu TFF wanapendelea wimbo wa “Tusifu sana, tufurahi”. Bahati mbaya sina uwezo wa kupiga midundo yake, najua ule wa “Lazima mtabadilika, hamuwezi, kaeni kando”.

Ndiyo maana nasema hivi; nitaendelea kuwapigia gitaa TFF na watu wake kwamba wao si watu sahihi ambao hawataki kuambiwa ukweli na ndiyo maana hawabadiliki na wakati mwingine wanafanya madudu ya hovyo kama hilo la kuiruhusu Azam FC kwenda kucheza Bonanza Zambia na kuacha Ligi Kuu Bara ikiendelea.

Malinzi ameonyesha uungwana, jana mbele ya waandishi wa habari ameomba radhi, amesema hata wakati wanaamua yeye alikuwa safarini nje ya nchi. Siku ya mwisho hawezi kukwepa hilo kwa kuwa yeye ndiye aliyehusika na kupatikana kwa watendaji wengi ambao wanaendelea kubaki TFF si kwa uwezo badala yake ushikaji.

Nimekuwa nikilia na watendaji wengi wa TFF kama mshauri wa ufundi wa rais wa shirikisho, msaidizi wa rais, mkurugenzi wa mashindano na wengine.

Hili la Azam FC, linaonyesha wazi lilihusisha watu ambao hawana uzoefu, wasiokuwa na uwezo mkubwa wa kutafakari haraka na kuangalia madhara ya baadaye baada ya kuwa ruhusa imetolewa.
Kama Malinzi kweli hakuwepo, bado TFF ilipaswa kubaki salama kama watendaji wangekuwa ni bora. Kitendo cha kusema walipoamua hakuwepo ni sehemu ya kukiri kwamba watendaji waliopo, hawakuwa makini na huo ndiyo ukweli.

 Umewahi kuona wapi, kiongozi wa shirikisho anafikia kuamini ligi haina thamani kwa bonanza. Umewahi kusikia lini kiongozi wa shirikisho anakubali kuvuruga ratiba ya ligi ili timu ikashiriki michuano fulani ya kujifurahisha?

Tunajua kuna michuano ya aina tatu ya ukanda na mmoja wa kitaifa ambayo inaweza kusimamisha ligi ya Tanzania Bara. Moja ni Kagame kwa upande wa klabu, pili ni Chalenji kama ikibidi na tatu ni Mapinduzi Cup ambayo ni ya kitaifa.

Sasa ligi inasimamishwa tena na michuano ya kirafiki ya Zambia. Itafikia kila mara na ligi itasimama hata mara tano kwa ajili ya michuano ya Zambia, Sudan, Afrika Kusini na kwingineko.

Vipi kiongozi wa shirikisho anashindwa kujua thamani ya ligi kuu ya nchi yake? Hii ndiyo ninasema ni kutokuwa na watu sahihi na kuendekeza ushikaji.

Nimesema nitaendelea kumpigia gitaa Malinzi, lengo langu ni kutaka aelewe na kukubali. Lengo langu ni kutaka akumbuke kwamba kuendekeza ushikaji ni kufeli. Kuendekeza ushikaji ni kukubali huna nia ya maendeleo lakini unataka kufurahisha nafsi tu.

TFF hii tuliyonayo, kupata ligi bora, yenye ushindani wa juu na heshima kubwa, tusahau. Itapatikana tu kama haya mawili yatatokea. Moja; Malinzi kukubali kubadilisha watu na kuwapa nafasi walio sahihi hata kama si washikaji zake, au mwenyewe kukubali kuondoka kabisa ili wengine waendeleze mpira kwa njia iliyonyooka yenye malengo sahihi yanayotekelezwa.

Waswahili wanasema hivi; “Mambo humnogea mwenye saburi”. Saburi ni subira, mimi sitachoka ntaendelea kukukumbusha hadi utakapoelewa na maendeleo yapatikane kwa kuwa najua inawezekana lakini uliowapa nafasi, hawana uwezo.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic