January 29, 2016



Na Saleh Ally
NAFIKIRI utakuwa unakumbuka kwamba Simba kwa sasa haina kocha wa makipa. Mara ya mwisho alikuwa ni Iddi Salim, raia wa Kenya, ambaye tayari amefutwa kazi.

Uongozi wa Simba ulimuondoa Salim pamoja na bosi wake, Dylan Kerr, raia wa England, baada ya uongozi kushindwa kuvumilia mwendo wa timu yao licha ya kwamba ilikuwa katika nafasi ya pili.
Tangu Simba imechukuliwa na aliyeajiriwa kama kocha msaidizi, imeshinda mechi tatu. Mbili za Ligi Kuu Bara, dhidi ya Mtibwa Sugar ilishinda bao 1-0 halafu ikaifunga JKT mabao 2-0.

Mechi ya tatu ilikuwa ni Kombe la FA, ikasafiri hadi Morogoro na kuitwanga Burkina Faso kwa mabao 3-0, imesonga mbele. Maana yake ndani ya mechi tatu, imefunga mabao sita, bila ya kufungwa hata moja na ushindi wa mechi zote tatu, ok, ni jambo zuri.

Wakati Simba ikiwa na kocha huyo msaidizi, Jackson Mayanja ambaye imeelezwa kwamba sasa atakuwa kama kocha mkuu wa muda, kuna jambo ambalo nimeamua kuwakumbusha viongozi wa Simba kama watakuwa tayari kulifanya, basi inawezekana kulifanya.

Moja ya sifa kubwa za Simba ni kuwa na vipaji vya juu, utaona wachezaji wake wengi, hasa vijana huanzia au kupitia Simba. Wengi wao wamekuwa wakifanya vizuri na hilo halina ubishi.

Ukiachana na wachezaji ambao naona sina haja ya kutoa mfano, Simba inasifika kwa kuwa na makocha ambao wana “damu” ya Msimbazi, jambo ambalo ni bora na linaaminika sana katika soka sehemu yoyote duniani.

MGOSI

Nitaanza na mfano kwanza na huenda utakumbuka huu ndiyo umekuwa mara nyingi mfumo wa Simba. 

Manchester United kwa sasa, Kocha Mkuu ni Louis van Gaal, msaidizi wake ni Ryan Giggs, huyu ni “damu” ya Manchester United. Ukienda Madrid, wakati fulani alikuwa Kocha Mkuu, Carlo Ancelotti, msaidizi wake ni Zinedine Zidane na sasa ndiye bosi mwenyewe.

Simba inajulikana namna ilivyoanza kuwapa nafasi wachezaji wake na baadaye wakawa makocha gwiji kama Abadallah Kibadeni ‘King’ na baadaye Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye hakuna anayeweza kubisha kwamba ni kati ya makocha wazuri na unaweza kuwapa timu wakafanya wanavyotaka.

Baada ya hapo, Simba ilimpa nafasi kocha mwingine, huyu ni Selemani Matola ambaye ana kipaji na uwezo mkubwa. Nafikiri wazo la kuondoka Simba lilikuwa zuri kwake, sasa ana nafasi ya kuonyesha uwezo wake akiwa huru na tunaona timu yake ya Geita Gold Sports inavyotikisa Ligi Daraja la Kwanza, acha tu arejee Ligi Kuu Bara akiweza.

Wakati hao wameondoka Simba, kuna Mayanja ambaye hana msaidizi tena wala bosi, kumbuka pia hana kocha wa makipa kama Simba ilivyowahi kutoa nafasi kwa watu kama akina Iddi Pazi au Patrick Mwangata ambaye sasa ni kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar.

Nani anafuata baada ya hao, Simba wanaliona hilo au wamesahau kabisa? Basi mimi nawakumbusha kuwa huu ndiyo wakati wa kuwaamini wengine kwa mara nyingine, mfano mzuri ni Juma Kaseja na Mussa Hassan Mgosi. Nitakueleza kwa nini.

Kaseja ni kocha wa makocha, kocha anayeendelea kucheza na tunajua makipa waliopita katika mikono yake wakifanya kazi pamoja kama Ally Mustapha ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na wengine wengi, sasa wanafanya vema.

Mgosi anakwenda anaisha ingawa bado yuko vizuri tu, lakini ana nafasi ya kuchukua nafasi ya kocha msaidizi hata kama ataamua kuwa kocha mchezaji bado inawezekana.

Kaseja na Mgosi ni wachezaji wenye nidhamu, heshima na kazi yao na hii ndiyo siri ya wao kuendelea kucheza hadi sasa wakiwa na viwango vizuri. Sasa Simba inasubiri nini wakati inaondoka katika mfumo wake?


Najua, inawezekana viongozi walisahau au walikuwa wanajivuta katika hili, ndiyo maana nawakumbusha vizuri kuendelea na utamaduni huo wa kujenga makocha wengine na wengine, hasa ambao wanaonyesha kuwa na vipaji. Mgosi na Kaseja wanaweza kuwa mfano, lakini Simba ina uwezo wa kuwa na wengine wengi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic