Kampuni ya Bilion Group ya Afrika Kusini, ipo tayari kuwekeza kwenye eneo la Uwanja wa Taifa, Dar ili kuufanya uwanja huo kuwa wa kimataifa zaidi kama vilivyo viwanja vingine duniani.
Kampuni hiyo inatarajiwa kujenga viwanja viwili vya michezo tofauti na soka pamoja na hosteli kubwa ambayo itatumiwa na timu mbalimbali zitakazokuja kucheza uwanjani hapo ili mapato yote yaingie serikalini.
Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, amesema hayo juzi ambapo alieleza kuwa ameshapokea maombi hayo ya wawekezaji na tayari ametuma ujumbe kwenye wizara husika ya michezo inayoongozwa na Waziri Nape Nnauye kwa ajili ya mazungumzo.
“Kuna watu wanaona mbali sana, kuna kampuni moja ya Afrika Kusini ya Bilion Group ililiangalia hili eneo la Uwanja wa Taifa ambalo lipo wazi na kuchora michoro yao kabisa, wakaona panafaa kwa kufanya uwekezaji, walipomaliza wakatufuata wakitaka kufanya hivyo ili kuiongezea mapato serikali.
“Wamesema wanataka kujenga viwanja viwili vya ‘in door’ kwa ajili ya michezo mbalimbali kama netiboli, kikapu, volleyball na mingine mingi,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Eneo ambalo linatakiwa kufanyiwa uwekezaji ni lile lililopo pembeni mwa Uwanja wa Uhuru mpaka zilipo ofisi za zamani za Baraza la Michezo Tanzania (BMT).
Waziri Majaliwa alisema hayo alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali wa michezo nchini wakiwemo viongozi na waandishi wa habari ndani ya Uwanja wa Taifa, juzi.








0 COMMENTS:
Post a Comment