Msemaji wa Simba, Hajji Manara amesema atamfikisha mtani wake Msemaji wa Yanga, Jerry Muro kwenye vyombo vya sheria.
Manara amesema atafikia huko kumfikisha polisi ikiwezekana kumpandisha kizimbani kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halitalifanyia kazi jambo hilo.
Manara ametoa kauli hiyo jana Alhamisi, ambapo alieleza masikitiko yake kwa kuwa TFF, imekuwa ikikaa kimya na kushindwa kumchukulia hatua zozote Muro kwa kauli za kudhalilisha huku akihoji rundo la kesi za Simba zilizopo TFF kutotolewa uamuzi.
Pamoja na kesi yake na Muro, Manara pia aliikumbushia kesi za Simba zilizo TFF kama ile ya Donad Ngoma kumpiga kichwa Hassan Kessy katika mchezo wa raundi ya kwanza, lakini hadi leo kimya na TFF wanasikia malalamiko yao wanaendelea kujikausha.
“TFF bila hata Simba kusema lolote, wao wenyewe walitangaza kumchukulia hatua za kinidhamu Muro kwa lugha ya kibaguzi, kudhalilishana lakini hakuna kilichofanyika.
“Muro amewahi kumdhalilisha kiongozi mmoja wa bodi ya ligi (Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Fatuma Abdallah), akawatukana Kimondo FC, kesi yangu ipo pale, kwanini jamani?
“Kama mnakumbuka, tuliwasilisha malalamiko kuhusu Ngoma kumpiga kichwa Kessy, kesi yetu katika sakata la Messi (Ramadhani Singano) lakini hakuna kilichofanyika kunanini? Sasa katika hili tumechoka na iwapo kamati ya maadili itashindwa kuchukua hatua, tusilaumiane.
“Tutakwenda polisi, tulitaka haya mambo yaishe kimichezo lakini kama hawatachukua hatua, litafika polisi,” alisema Manara.
0 COMMENTS:
Post a Comment