February 19, 2016



Na Saleh Ally
KUNA ujanja mwingi sana umetengenezwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kuhakikisha kunakuwa na njia rafiki ya kulinda maovu yao ya ubadhirifu na matakwa binafsi.

Fifa imetengeneza mfumo wa shirikisho hilo kutoingiliwa na uongozi wa serikali mbalimbali duniani kote.

Mfumo huo ndiyo unalilinda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwamba likikosolewa au kuadhibiwa na serikali, basi litakuwa limeingiliwa. Kwangu huwa ninaona huu ni upuuzi mkubwa wa karne.

Tanzania inafanya maendeleo ya soka kwa watu wake, aliye pale amechaguliwa na Watanzania. Halafu inaonekana hafai, lakini hataguswa hadi hapo atakapomaliza muda wake. Nasema hivi, hii si sawa na kuna kila sababu ya serikali ya nchi mbalimbali kuliangalia.

Methali moja ya Kiswahili inasema hivi; “Elimu bila asili ni ujahili”. Hauwezi kuwa una elimu ya kitu fulani halafu usiwe na nidhamu na ukafanikiwa. Mchezaji mwenye kipaji kama hana nidhamu hawezi kufanikiwa.

Ndani ya TFF, tunajua watu hawana nidhamu ya mambo muhimu na hii ni sehemu ya kuonyesha ugumu wa juu kabisa wa mafanikio. Tutabaki tukipiga hatua moja mbele na kurudi tatu huku tukiamini serikali kuingilia kuzuia uozo ni sawa na kuiingilia TFF. Kama ni hivyo basi hiyo TFF ihamie kwenye ‘nchi’ ya Fifa.

Hivi karibuni, tumeona viongozi mabazazi wa Fifa akiwemo Rais Sepp Blatter wakitumbuliwa majipu na ule mfumo na mtandao wao wa ulaji fedha za mpira ambazo si mali zao, umechanwachanwa. Watu wamechoka, sasa vipi hapa nyumbani hatuchoki na TFF?

Nimefikia kuandika haya baada ya kuona Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akichukua uamuzi sahihi kabisa wa kukutana na viongozi mbalimbali wa vyama na mashirikisho ya michezo nchini.

TFF nao walikuwepo, wakiwakilishwa na rais wao, Jamal Malinzi na viongozi wengine. Kitaaluma, Majaliwa pia ni kocha. Ni mpenda mchezo na anajua mengi kuhusu michezo.

Ndiyo maana ilikuwa rahisi kwake kujua kuwa ofisi za Chama cha Makocha Tanzania (Tafca), zimevunjwa. Hazipo tena na TFF inasema ina mpango wa kukuza vijana huku ikionyesha dharau kwa wadau wake muhimu sana.

Eti bora kuweka duka la kuuza jezi, kuliko kuwa na ofisi za Tafca. Sasa wanatumia ofisi ya Ofisa Michezo wa Manispaa ya Ilala, Michael Bundala ambaye ni katibu mkuu wa Tafca.

Makocha hawana ofisi, wanadandia ofisi za watu, huku wakipewa ahadi kila siku kutafutiwa ofisi. Halafu unataka mpira uendelee na unazungumzia kukuza vijana. Huu ni upuuzi wa hali ya juu kabisa.

Lakini Waziri Mkuu Majaliwa anajua kuwa Kocha Kim Poulsen alifukuzwa, halafu Malinzi amesema anarudishwa. Ndiyo maana amehoji imekuwaje, aliondoka? Sasa anarudishwa na kama ni kweli hayo ni matakwa ya taasisi au mtu mmoja.

Wadau wanakumbuka, alifukuzwa bila sababu, kisa, utawala mpya umeamua! Akalipwa mamilioni ya fedha za udhamini wa Taifa Stars. Akaajiriwa Mart Nooij kwa mamilioni ya fedha hizo, kocha hovyo kabisa. Halafu naye akafukuzwa akalipwa mamilioni.

Leo Poulsen anarudishwa, tena analipwa mamilioni. Huu ni ubadhirifu mkubwa kabisa. Hili ni jipu.

Waziri mkuu amezungumzia suala la tiketi za elektroniki. Hizi zilikuwa na mtandao mkubwa hadi ndani ya wizara, wako walihalalishaji “upigaji”, najua matatizo yanawakuta sasa.

Najua Waziri Mkuu Majaliwa alilisahau suala la Dk Damas Ndumbaro ambaye alifungiwa “kihuni” kabisa. Kisa alikuwa anazitetea klabu kukataa jambo ambalo si sahihi, kafungiwa miaka mitano, hakuna anayemtetea kwa kuwa Fifa inailinda TFF, serikali yetu na Fifa ipi sahihi kwetu?

 Lakini naona hata Waziri Mkuu Majaliwa amesita kuitumbua TFF kwa sababu ya ule mfumo “linda” wa Fifa, lakini kwa hali halisi, alitakiwa kufanya jambo zaidi ya vile.

TFF ni tatizo, mambo mengi yanakwenda kwa matakwa ya watu binafsi na kuwalinda wenyewe. Si kwa maendeleo ya mpira. Mimi nimesema mara nyingi karibu na zaidi ya alichokisema Waziri Mkuu Majaliwa, imekuwa ikionekana nawasakama TFF.
Waziri mkuu pia anayajua hayo, naye anawaonea au anawasakama TFF? Wale ambao wanaunga mkono madudu yao, sasa waone haya, tuungane kuwaeleza ukweli kuupigania mpira wa Tanzania. Ninaamini umefika wakati wa kuuacha nyuma mfumo “linda” wa Fifa na kutumbua majipu ya TFF ili tuusaidie mpira wetu, jamani chokeni kuwa wa mwisho.



1 COMMENTS:

  1. Mbona Simba kuna Tambazi(jipu kubwa kupita kiasi) na bado TFF wamekataza tusilitumbue?Huo ndio mpira sasa kama mtu anaona sheria hiyo haifai basi ajiondoe kushabikia futiboli kwani ipo michezo mingi ya kushabikia kama dhumna nk.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic