Ushindi mtamu, bingwa wa Mabara, bondia Mtanzania, Francis Cheka anataka kuchukua mkanda wake wa ubingwa na kuufikisha kwa Rais John Pombe Magufuli.
Cheka amefanikiwa kuutwaa mkanda huo baada ya kumshinda bondia matata kabisa, Geard Ajetovic raia wa Serbia anayefanya kazi zake nchini Uingereza.
Katika mkutano na waandishi wa habari katika Hotel ya The Atriums jijini Dar es Salaam, Cheka amesema kuwa ataupeleka mkanda wake kwa Rais Magufuli kwa kuwa anataka kuongeza hamasa ya kuunga mkono mchezo wa ngumi.
“Nastahili pongezi kwa uwakilishi wangu mzuri, nimepigana na bondia mwenye kiwango cha juu kabisa na leo nimeshinda. Mkanda huu ni kwa Watanzania wote kama mabingwa.
"Lakini ningependa kuufikisha kwa mheshimiwa Rais Magufuli ikiwa ni sehemu ya kuonyesha kwamba ninaikubali serikali yake, pia naomba iendelee kuupa mchezo wa ngumi sapoti zaidi ya hapa," alisema Cheka.
"Ilianza kwa Samatta (Mbwana) aliyetwaa uchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa Afrika, sasa hivi ni zamu yangu. Nimeshinda mkanda wa Mabara, ni jambo la sisi Watanzania kujivunia."
Hata hivyo, Cheka alikiri, mpinzani wake alikuwa na kiwango cha juu kabisa na ulikuwa upinzani mkali alioupata.







0 COMMENTS:
Post a Comment