Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kimekamilika baada ya kundi la pili lenye wachezaji nane kuwasili leo mchana nchini Chad tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya wenyeji kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 2017.
Kundi hilo la pili limewasili majira ya saa sita mchana (saa za Chad) likiongozwa na mkuu wa msafara ambaye pia ni Rais za ZFA, Ravia Idarus na kupokelewa na viongozi waliopo jijini N’Djamena.
Mara baada ya kuwasili D’jamena wachezaji walipata nafasi ya kupumzika hotelini kabla ya kuelekea mazoezini kufanya mazoezi ya pamoja kwa wachezaji wote, yakiwa ni mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo wa kesho.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars Charles Mkwasa amekiongoza kikosi chake chenye jumla ya wachezaji 20 kufanya mazoezi mepesi saa 9 mchana katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya uliopo jijini N’Djamena.
Katika mazoezi ya leo wachezaji wa Taifa Stars walionekana kuwa na umakini mkubwa katika kusikiliza maelekezo ya kocha Mkwasa, huku morali ya wachezaji ikiwa juu kuelekea kusaka pointi 3 muhimu katika mchezo huo.
Wachezaji waliopo Chad ni magolikipa Aishi Manula na Ally Mustafa, walinzi Shomari Kapombe, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Mohamed Hussein, David Mwantika, Erasto Nyoni na Kelvin Yondani.
Viungo ni Himid Mao, Jonas Mkude, Mwinyi Kazmito, Mohamed Ibrahim, Farid Musa, Deus Kaseke na Shiza Kichuya, huku washambuliaji wakiwa ni John Bocco, Ibrahim Ajibu, Thomas Ulimwengu na nahodha Mbwana Samatta.
Mechi kati ya Chad dhidi ya Tanzania inatarajiwa kuchezwa kesho Jumatano saa 9:30 (saa 11:30 kwa saa za Tanzania) katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya jijini N’Djamena, na utarushwa moja moja na kituo cha luninga cha Taifa cha Chad (Tele Chad).
0 COMMENTS:
Post a Comment