March 14, 2016Washambuliaji watatu nyota wa Yanga, Simon Msuva, Amissi Tambwe na Donald Ngoma waliopewa jina la utani la MTN, bado wana deni kuhakikisha wanaivusha Yanga katika mechi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga inakutana na APR wikiendi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kuwa imepata ushindi wa mabao 2-1 ugenini.

Hata hivyo, ushindi huo hauihakikishii Yanga ushindi kwa kuwa APR bado ni timu nzuri na inaweza kubadilika.

MTN ambao walikuwa gumzo katika jiji la Kigali, hawakuonyesha cheche zao. Tambwe alikuwa majeruhi, alishindwa kucheza vizuri katika dakika 45 za kwanza, akatolewa. Msuva aliingia baadaye bado hakufanya vema.

Ngoma aliyekuwa ndani kuanzia mwanzo, naye hakuwa tihishio sana na mabao mawili ya beki Juma Abdul na kiungo Thabani Kamusoko ndiyo yakaiokoa Yanga.

Yanga inahitaji angalau mabao mawili au ushindi wa aina yoyote kujihakikishia kusonga mbele. Bado sare inaweza kuwa nzuri lakini haipaswi kuwa lengo namba moja. Hivyo MTN ndiyo wanaoweza kurahisisha mambo kama wakiamua.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV